Ufaransa: Mshirika wa mshambulizi wa Nice atiwa mbaroni
30 Oktoba 2020Mtu mwenye umri wa miaka 47 ambae amedhaniwa kushirikiana na mshambuliaji aliewauwa watu watatu kwa kisu hapo jana nchini Ufaransa amekamatwa. Duru za kisheria nchini humo zinasema Ofisi ya mashtaka dhidi ya Ugaidi (Pnat) imefungua uchunguzi wa "mauaji na jaribio la mauaji kwa ushirikiano na kundi la kigaidi" na "kundi la magaidi wahalifu".
Hadi sasa hakujatolewa maelezo zaidi kuhusu utambulisho wa mtu huyo aliyekamatwa na polisi usiku wa kuamkia leo mjini Nice kusini mwa Ufaransa. Duru za kisheria zinaelezea kwamba mtu huyo aliyekamatwa alikutana na mshambuliaji siku moja kabla ya tukio. Lakini hata hivyo haijulikani ikiwa alihusika katika kupanga mashambulizi hayo.
Jean-Francois Ricard, mwendesha mashtaka wa kitengo cha kupambana na ugaidi nchini Ufaransa,amesema kuwa uchunguzi umeendesha kuhusu mauwaji.
'' Kutokana na mazingira ya mashambulizi hayo, ofisi ya mwendesha mashtaka wa kupambana na ugaidi, imeanzisha uchunguzi kuhusu mauwaji na jaribio la mauwaji kwa kushirikiana na kundi la kigaidi.''
Watu watatu waliuliwa Alhamisi asubuhi katika shambulio lililotokea katika kanisa la Notre-Dame huko Nice, Kusini mwa Ufaransa. Mshambuliaji alijeruhiwa na kukamatwa, kulingana na msemaji wa polisi.
Mshambuliaji ni mhamiaji kutoka Tunisia
Mshambuliaji huyo ambae ni raia wa Tunisia mwenye umri wa miaka 21,aliingia barani Ulaya kupitia kisiwa cha Lampedusa,Italia ,Septemba 20.
Kwenye begi lake liliokutwa kwenye eneo la tukio, mshambuliaji huyo aliyetambuliwa kama Brahim Aouissaoui alikuwa na msahafu, simu mbili na kitambulisho cha shirika la msalaba mwekundu la Italia. Inaaminika kwamba aliingia nchini Ufaransa tarehe 9 Oktoba.
Kufuatia tukio hilo, Waziri Mkuu wa Ufaransa ametangaza kuongeza kiwango cha hali ya tahadhari nchini humo hadi cha juu zaidi. Kikao cha dharuira cha usalama kimeitishwa leo Ijumaa na Rais Macron.Macron amesema shambulizi hilo lilikuwa la ugaidi wa kiislamu.
Ni shambulio la tatu katika kipindi cha miezi miwili, huku Ufaransa ikiwa inakabiliwa na ukosoaji mkubwa kutoka katika mataifa ya Kiislam, kuhusu vibonzo vya Mtume Muhammad vilivyochapishwa tena na gazeti la nchini humo Charlie Hebdo.
Macron alisema wazi kwamba Ufaransa haitaacha kuchora vibonzo, kufuatia kuchinjwa kwa mwalimu Samuel Paty aliyewaonyesha wanafunzi wake kibonzo cha Mtume Muhammad mapema mwezi huu.
Viongozi kadhaa duniani,akiwemo Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, wali laani mashambulizi hayo ya jana.