Ufaransa na G5 kufanya mkutano wa kilele kuhusu ugaidi
15 Februari 2021Ufaransa pamoja na washirika wake watano wa eneo la Sahel wanakutana hii leo kujadiliana kuhusu uasi unaoendelea kwenye eneo hilo, katika wakati ambapo serikali ya mjini Paris ikiangazia uungwaji mkono utakaoiwezesha kupunguza wanajeshi wake katika eneo hilo lililoharibiwa na mashambulizi ya waasi.
Wakuu wa kundi hilo la G5 Sahel kutoka Burkina Faso, Chad, Mali, Mauritania na Niger wanahudhuria mkutano huo wa kilele wa siku mbili katika mji mkuu wa Chad, N'Djamena.
Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa atahudhuria mkutano huo kwa njia ya video. Mkutano huo unafanyika mwaka mmoja baada ya Ufaransa kuimarisha vikosi vyake kwenye eneo la Sahel, ikiwa ni sehemu ya kupunguza kasi ya uasi uliodumu kwa muda mrefu kwenye eneo hilo.
Hata hivyo licha ya mafanikio hayo ya kujiimarisha kijeshi, waasi wamesalia na udhibiti wa eneo kubwa pamoja na kuendeleza mashambulizi yasiyokoma.
''Sio Ufaransa itakayo tatua taizo la usalama''
Jean-Hervé Jézéquel, mtafiti mkuu wa Sahel kwenye shirika la kupambana na mizozo, ICG amesema kuwa bado changamoto ni nyingi kwa nchi za Sahel ili kukomesha ugaidi.
'' Sio Ufaransa itakayo tatua matatizo ya kiusalama ya eneo la Sahel. Uwepo wa wanajeshi wa Ufaransa utaendelea kuchochea mzozo kwa wale wanaosema nchi zao zinavamiwa na vikosi vya nje. Endapo wanajeshi wa Ufaransa na Umoja wa Mataifa wataendelea kuwepo mzozo huo hautomalizika. Viongozi wa kikanda wanatakiwa kubeba majukumu yao wenyewe ilikukomesha mzozo huo.''
Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa,Jean-Yves le Drian alisema mapema leo kwamba mkutano huo wa Ndjamana unatarajiwa kujadili hasa maswala ya kidiplomasia.
Kabla ya kufunguliwa kwa mkutano huo,nchi ya Mali ilidai fedha zaidi kwa ajili ya mapambano yake dhidi ya ugaidi. Naibu Waziri wa mambo ya nje wa Mali Boubacar Gouro ameliambia shirika la habari la DPA kuwa wanakabiliwa na changamoto za ufadhili.
Ujermani na Ufaransa zaunga mkono G5 Sahel
Mbali na Umoja wa Mataifa, Ujerumani na Ufaransa zinaunga mkono juhudi za nchi wanachama wa ukanda wa Sahel katika oparesheni za kupambana na ugaidi.
Mkutano huo unajiri mwaka mmoja baada ya ule uliofanyika Januari 13, katika mji Pau, kusini mwa Ufaransa, ambao viongozi wa Ufaransa na Afrika Magharibi waliapa kuongeza juhudi za pamoja za kijeshi katika ukanda wa Sahel.