1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa na Ujerumani zasisitiza ushirikiano wao

Sekione Kitojo
24 Juni 2017

Emmanuel Macron na Angela Merkel wametumia mkutano wa kwanza wa kilele wa rais huyo wa Ufaransa katika Umoja wa Ulaya Ijumaa(23.06.2017)kutuma ujumbe usio na shaka:nchi zao zina nia ya kuungoza Umoja huo baada ya Brexit.

https://p.dw.com/p/2fJ3s
EU-Gipfel in Brüssel | Angela Merkel & Emmanuel Macron
Picha: Reuters/G. Fuentes

Viongozi  hao  wawili  wa  Ujerumani  na  Ufaransa  walikuwa  na  mkutano  usio  wa  kawaida wa  pamoja  na  waandishi  habari baada  ya  kukutana  na  wenzao 26 wa  Umoja  wa  Ulaya.

"Wakati  Ujerumani  na  Ufaransa  zikizungumza kwa  sauti  moja, Ulaya  inaweza kusongambele," rais mpya  Macron  aliwaambia  waandishi  habari  waliojazana  katika chumba  cha  mkutano  wakati  akisimama  pamoja  na  kansela  wa  Ujerumani.

	EU Gipfel Angela Merkel Ankunft
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel Picha: Reuters/E. Vidal

"Hakutakuwa na suluhisho  la mfungamano  iwapo sio  suluhisho la  mfungamano kwa Ufaransa  na  Ujerumani," kiongozi  huyo  mwenye umri  wa  miaka  39  anayefuata  siasa  za wastani  za  mrengo  wa  kati  alisema.

Licha  ya mtazamo  wake  wa  nadharia  za  vitendo  zaidi , ujumbe  kutoka  kwa  Merkel mwenye  umri  wa  miaka 62 ulikuwa huo huo.

"Mkutano  huu  na  waandishi  habari  unaonesha  kwamba  tumeamua  kujiunga  pamoja kutafuta  suluhisho kwa  ajili  ya  matatizo," amesema  Merkel.

EU Gipfel Emmanuel Macron Ankunft
Rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: Reuters/G. Fuentes

Mkutano  huo  wa  pamoja  na  waandishi  habari  umekuja  mwaka  mmoja  kamili  baada ya kura ya kushitua  ya  maoni  kwa  Uingereza  kuwa  nchi  ya  kwanza  kujitoa  kutoka  Umoja wa  Ulaya , hali  iliyosababisha utabiri  wa  kuvunjika  kwa  Umoja  huo.

Ulaya  yaweka kando siasa kali

Lakini Ulaya  imepanda  katika  mkokoteni  wa  ushindi wa  kushitua  wa  Macron  dhidi  ya kiongozi  wa  siasa  kali  za  mrengo  wa  kulia  nchini  Ufaransa  Marine Le Pen  na  kupuliza tarumbeta  la  matumaini  baada  ya  miaka  ya  kubana  matumizi na  mzozo licha  ya   kujitoa kwa  Uingereza,  Brexit.

EU Gipfel Theresa May Ankunft
Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May(kushoto)Picha: Reuters/G. Fuentes

Katikati  ya  hilo kuna  wazo kwamba  macron  huenda  atafanikiwa  kuufanyia  ukarabati "moyo" wa  utamaduni  nyuma  ya  ujumuisho  wa  Ulaya , ushirikiano  wa  baada  ya  vita  wa Ufaransa  na  Ujerumani  baada  ya  karne  kadhaa  za  mizozo.

Viongozi  wa  Ufaransa  na  Ujerumani , wengi  wakiuita  kwa  jina  la  utani  Merkron , Mackerel  na  Emmangela  ni mtindo wa  majina  ya  utani  ya  watu  hao  maarufu, kusema wanania  ya  kutumia nguvu  hizo kusonga mbele.

Macron  amesisitiza kuhusu umoja  wao  katika  masuala  kadhaa  ikiwa  ni  pamoja  na kuimarisha  uwezo  wa  kiulinzi  wa  bara  la  Ulaya , wakati  bara  hilo  likishindwa kuzitegemea  Uingereza ama  Marekani  chini  ya  Donald  Trump.

Baada ya Marekani kuitupa mkono Ulaya

Pia  wametangaza  kuwapo  kwao pamoja  kuhusiana  na  suala  la  mabadiliko  ya tabianchi, hususan  baada  ya  Trump kujitoa kutoka  mkataba  wa Paris wa  mazingira, mapambano  dhidi  ya  ugaidi  na  masuala  ya  biashara.

Hata  hivyo walikuwa  waangalifu  kwa  kukwepa  kuingia  ndani  zaidi  kutoa  maelezo  katika masuala  nyeti kama  mageuzi ya  kanda  ya  euro, mradi maalum wa  Macron  ambaye anataka  nchi  hizo  ziwe  na  bunge  lake  lenyewe  pamoja  na  waziri  wa  fedha.

Donald Trump und Jared Kushner
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Getty Images/AFP/M. Ngan

"Hatutangazi mapema  mambo  ambayo  hatuwezi  kuyaendeleza," alisema  kansela  Merkel ambaye  mara  nyingi  ni  mtu  anayesema  jambo  la  maana, wakati  alipoulizwa  iwapo hatimaye wataamua kutumia mapendekezo kamili  baada  ya  uchaguzi  wa  Ujerumani mwezi  Septemba.

Viongozi  hao  wawili  pia  walichukua  msimamo  wa  tahadhari  kuelekea  waziri  pendekezo la  waziri  mkuu  wa  Uingereza  Theresa  May  kuhusiana  na  haki  ya  raia  wa  Umoja  wa Ulaya  wanaoishi  nchini  Uingereza  baada  ya  mchakato  wa  Brexit.

Lakini  katika  eneo  moja, Macron huenda  aligundua  kwamba  fungate  ya mkutano  huo ilikuwa  imekwisha kabla  ya  kuanza.

Mwandishi:   Sekione  Kitojo / afpe

Mhariri:  Yusra Buwayhid