Ufaransa: Rufani ya rais wa zamani Nicolas Sarkozy yatupwa
25 Oktoba 2018Baada ya rufani yake kukataliwa mahakamani siku ya Alhamisi Sarkozy anapaswa kufikishwa mbele ya mahakama kujibu mashtaka ya kuvuka kiwango cha fedha kinachoruhusiwa kwa ajili ya kuendeshea kampeni za uchaguzi.
Mnamo mwaka 2012 Sarkozy alitumia kiwango cha fedha kikubwa zaidi kuliko kile kinachoruhusiwa kisheria kwa ajili ya matumizi ya kampeni. Waendesha mashtaka wamesema kampuni ya mambo ya uenezi inayoitwa Bygmalion inatuhumiwa kuhusika na matumizi ya Euro milioni 22.5 kwa ajili ya bwana Sarkozy wakati wa kampeni za uchaguzi wa urais wa nchini Ufaransa mnamo mwaka huo wa 2012. Kwa mujibu wa taarifa kampuni hiyo ilijaribu kufunika njama hizo kwa kutoa stakabadhi bandia. Watu wengine 13 wanakabiliwa na mashtaka hayo pamoja na rais huyo wa zamani.
Sarkozy pia anakabiliwana mashtaka ya rushwa na kutumia vibaya mamlaka. Kuna madai kwamba mnamo mwaka 2014 Sarkozy alijipatia taarifa ya siri kutoka kwa mwanasheria mkuu kwa kupitia kwa wakili wake.
Pia anafanyiwa uchunguzi juu ya madai kwamba mnamo mwaka 2007 alipokea fedha kutoka kwa aliyekua rais wa Libya Muammar Gaddafi kwa ajili ya kuendeshea kampeni yake ya uchaguzi.
Hata hivyo wakili wake Thierry Herzog, amewaambia waandishi wa habari kuwa atakata rufaa katika mahakama ya juu. Kuna mahakama kama hizo nne zenye uwezo wa kutoa maamuzi ya mwisho nchini Ufaransa. Bwana Sarkozy pia anakabiliwa na tuhuma za hongo na ushawishi kinyume cha sheria au kutumia mamlaka vibaya.
Rais wa zamani wa Ufaransa Nicholas Sarkozy amekanusha mashtaka hayo, akisema yeye hakujua udanganyifu uliofanywa na watendaji wa kampuni hiyo ya Bygmalion. Wakuu wa kampuni ya Bygmalion na naibu meneja wa kampeni ya Sarkozy katika kampeni za mwaka 2012 Jerome Lavrilleux, wamekubali kuwepo kwa vitendo vya udanganyifu na pia uhasibu wa uwongo.
Nicholas Sarkozy alikuwa rais wa Ufaransa kuanzia mwaka 2007 hadi mwaka 2012. Alipojaribu kuwania muhula wa pili alishindwa na mgombea wa chama cha Kisoshalisti Francois Hollande.
Mwandishi:Zainab Aziz/DPAE/AFPE
Mhariri: Iddi Ssessanga