Ufaransa, Uingereza na AU walaani mapinduzi ya kijeshi Gabon
31 Agosti 2023Katika taarifa kwa vyombo vya habari, mwenyekiti wa kamisheni ya Umoja wa Afrika Moussa Faki ameyataja mapinduzi hayo ya kijeshi katika taifa hilo koloni la zamani la Ufaransa, kama ukiukaji wa wazi wa sheria ikiwa ni pamoja na mkataba wa Afrika kuhusu uchaguzi, demokrasia na utawala.
Faki ametoa wito kwa jeshi la Gabon kuhakikisha usalama wa Ali Bongo, jamaa zake na baadhi ya maafisa waliokuwa wakimuhudumia.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres pia ameelani mapinduzi hayo.
Kupitia taarifa, Guterres ametoa wito kwa wahusika wote kushiriki katika mazungumzo jumuishi na kuhakikisha kuwa utawala wa kisheria na haki za binadamu zinaheshimiwa.
Jeshi lilitwaa madaraka nchini Gabon mapema jana Jumatano. Maafisa wa kijeshi walitangaza kwenye televisheni ya kitaifa kuwa taasisi zote za serikali na matokeo ya uchaguzi yamefutwa kutokana na udanganyifu na kwamba mipaka ya nchi hiyo imefungwa.