1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa, Uingereza zakubaliana kuunda ndege zisizorubani

Admin.WagnerD3 Machi 2016

Ufaransa na Uingereza zimekubaliana kuwekeza zaidi ya Euro billioni 2 katika uundaji wa ndege zisizo na rubani zinazotumika katika mapigano baada ya mwaka 2030. Hayo yamefikiwa katika mkutano wa kilele

https://p.dw.com/p/1I6Tz
Francois Hollande na David Cameron katika kasri la Elysee
Francois Hollande na David Cameron katika kasri la ElyseePicha: Getty Images/T.Chesnot

Taarifa iliyotolewa kufuatia mkutano huo uliofanyika katika mji wa kaskazini mwa Ufaransa wa Amiens imeeleza kwamba nchi hizo mbili zimetiliana saini makubaliano ya kuwekeza katika mradi ya kuunda ndege za kisasa kabisa zisizo na rubani ambazo zinaweza kuanza kutumiwa baada ya mwaka 2030. Kadhalika katika mkutano huo wa kilele Ufaransa na Uingereza zimeitaka serikali ya Syria na washirika wake Urusi kukomesha mara moja mashambulizi dhidi ya waasi wanaungwa mkono na nchi za Magharibi zikiema pande zote nchini humo zimetekeleza kikamilifu hatua ya usitishaji vita na kuruhusu kufikiwa maeneo ambayo yamezingirwa.

Taarifa hiyo pia imeeleza kwamba mashambulizi dhidi ya raia na wafanyakazi wa shughuli za hospitali yanabidi yakome na kwamba serikali ya Syria na washirika wake wanatakiwa kusimamisha operesheni zao kuelekea mji wa Aleppo ambazo zinakwamisha hatua za kufikiwa amani na kutishia mgogoro wa wakimbizi kuongezeka huku dola la kiislamu likifaidika kutokana na hali hiyo. Ama kwa upande mwingine nchi hizo mbili zimeitaka Urusi kutumia ushawishi wake kuelekea waasi wa mashariki mwa Ukraine kusimamisha ghasia katika eneo hilo na kuitolea mwito vile vile serikali ya Ukraine kuziweka pamoja juhudi zake ili kuanza utekelezaji wa mageuzi.

Mkutano huo wa kilele kati ya Ufaransa na Uingereza ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 100 tangu mapambano ya kwanza ya vita vya dunia ya vikosi vya utawala wa Uingereza na Ufaransa dhidi ya Ujerumani vita ambayvo vikifahamika kama mapambano ya Somme ambapo wanajeshi 600,000 wa Uingereza na Ufaransa waliuwawa.

Bunge la Ulaya likijadili kile kinachoitwa Brexit
Bunge la Ulaya likijadili kile kinachoitwa BrexitPicha: Reuters/V. Kessler

Hata hivyo mkutano huo umekuja katika wakati ambapo mgogoro juu ya wakimbizi unazidi kutanuka huku pia mjadala kabambe ukishuhudiwa kuhusiana na suala la kura ya maoni juu ya kubakia au kutobakia Uingereza katika Jumuiya ya Umoja wa Ulaya.Awali waziri wa fedha wa Ufaransa Emmanuel Maron ambaye hakuhudhuria mkutano huo wa leo alisema wakati akihojiwa kwamba Ufaransa itaufungua mpaka wake na Uingereza na kuwaachia maelefu ya wahamiaji kuelekea Uingereza ikiwa nchi hiyo itapiga kura ya kujiondoa kwenye umoja huo wa Ulaya

Hata waziri mkuu wa Uingerez David Cameron binafasi ameonya kwambakujiondoa nchi yake katika Umoja huo huenda kukamaanisha mwisho wa makubaliano kati yake na Ufaransa,makubalino ambayo hadi sasa yamekuwa yakiilazimu Ufaransa kuudhibiti mpaka wake na nchi hiyo.

Mwandishi: Saumu mwasimba , afp

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman