1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa, Umoja wa Ulaya walaani mashambulizi Saudi Arabia.

15 Septemba 2019

Wizara ya mambo ya nje ya Iran imezipuuza shutuma za Marekani kwamba inahusika na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani katika vituo vya mafuta vya Saudi Arabia. Wizara hiyo imesema madai hayo hayana ''maana''.

https://p.dw.com/p/3PdM9
Saudi-Arabien Feuer in der Aramco-Ölaufbereitungsanlage in Abkaik
Picha: Reuters/Stringer

Msemaji wa wizara hiyo, Abbas Mousavi amenukuliwa akisema shutuma kama hizo hazieleweki na hazina maana na kwamba zinakusudiwa kuhalalisha hatua za kuchukuliwa hapo baadae dhidi ya Iran. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo aliishutumu Iran kuhusika na mashambulizi hayo yaliyofanyika jana.

Waasi wa Houthiwanaoungwa mkono na Iran nchini Yemen wamedai kuhusika na mashambulizi katika vituo hivyo vya mafuta vinavyoendeshwa na kampuni kuba ya mafuta ya Aramco jana Jumamosi.

Yemen, taifa masikini zaidi miongoni mwa mataifa ya ulimwengu wa Kiarabu, imejikuta katika mzozo mbaya wa madaraka kati ya Wahouthi na serikali inayoungwa mkono na Saudi Arabia tangu mwishoni mwa mwaka 2014.

Hata hivyo, Pompeo anapinga madai hayo ya Wahouthi ya kushambulia vituo hivyo. Aliandika kwenye ukurasa wake wa twitter kwamba "Tehran iko nyuma ya karibu mashambulizi 100 nchini Saudi Arabia, wakati rais wa Iran Hassan Rouhani na waziri wake wa mambo ya nje Mohammad Javad Zarif akijifanya kujihusisha na diplomasia". Aliongeza kuwa "Hakuna uthibitisho kwamba mashambulizi hayo yalifanywa kutoka Yemen".

USA Britischer Außenminister Dominic Raab in Washington
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo anakataa kwamba Wahouthi wanahusika na mashambulizi ya vituo vya mafuta vya SaudiaPicha: picture-alliance/dpa/S. Walsh

Mousavi naye aliandika akisema, "kwa kuwa sera ya Marekani ya kuibinya zaidi Iran imeshindwa, Wamarekani hivi sasa wamegeukia uwongo wa hali ya juu". Alisema, hata katika nyakati ngumu zaidi za mvutano wa wanasiasa, taarifa zinazotolewa zinatakiwa angalau ziwe zimethibitishwa.

Saudi Arabia, ambayo ni muuzaji mkubwa zaidi wa mafuta nje, imeshuhudia kupungua kwa uuzaji wake kwa mapipa milioni 5.7, siku moja baada ya mashambulizi hayo ya Jumamosi, hii ikiwa ni kulingana na Aramco.

Wakati huo huo, Ufaransa, imelaani mashambulizi kwenye vituo hivyo, ambayo yamekuwa na athari kwenye uuzaji wa mafuta duniani, hii ikiwa ni kulingana na taarifa iliyotolewa Jumapili na wizara ya mambo ya kigeni ya nchi hiyo. Taarifa ya wizara hiyo imesema "Ufaransa inalaani vikali mashambulizi ya Jumamosi kwenye vituo vya mafuta vya Abqaiq na Khurais." Taarifa hiyo pia iliongeza kuwa Ufaransa inasimama pamoja na Saudi Arabia.

Aidha, taarifa hiyo imesema "mashambulizi kama hayo yanaweza kuongeza hali ya wasiwasi ya kikanda na hatari ya kuzuka kwa mzozo, na kuwataka washambuliaji kusitisha mashmabulizi ya aina hiyo.

Umoja wa Ulaya umeonya kuhusu ''kitisho cha kweli cha usalama wa kikanda'' katika Mashariki ya Kati. Msemaji wa mkuu wa sera za kigeni wa umoja huo, Federica Mogherini amesema mashambulizi hayo yanadhoofisha juhudi zinazoendelea za kuleta utulivu kwenye eneo hilo.