Ufaransa yaimarisha ulinzi na usalama
15 Juni 2016Maafisa nchini Ufaransa wanasema kwamba mtu mwenye itikadi kali aliewahi kutiwa hatiani huko nyuma, na ambaye alimuua afisa wa polisi na mke wake katika shambulizi la kisu lililohamasisha na kundi la Dola la Kiislamu, alikuwa amebeba orodha ya walengwa mashuhuri wa mashambulizi, na kuwahimiza wafuasi kuyageuza mashindano ya Euro 2016 kuwa "makaburi."
Shambulio la siku ya Jumatatu katika mji mdogo kaskazini magharibi mwa Paris ni la kwanza tangu kutokea kwa mashambulizi yaliyotekelezwa na IS mwezi Novemba na kuua watu 130.
Kufuatia mashambulizi hayo ya kitongoji cha Magnanville, polisi wanasema maafisa wake sasa watapaswa kubeba silaha wakati wakiwa nje ya majukumu ya kazi kwa ajili ya tahadhari inayoweza kujitokeza.
Katika shambulio la usiku wa Jumatatu, mshambuliaji Larossi Abballa aliyekuwa akifuatiliwa baada ya kutumikia kwa muda na wanajihadi, aliwaua kwa kuwachoma kwa kisu kamanda wa polisi Jean-Baptiste na mke wake nje ya nyumba yao.
Walengwa wa shambulio
Mwendesha mashitaka wa Paris Francois Molins amesema kwamba Abballa anayetoka kitongoji cha jirani cha Monte-la-Jolie aliwaambia polisi kuwa "muuaji alisema kwamba yeye ni Muislamu na alikuwa akitimiza Ramadhan, alisema kuwa alikuwa amekula kiapo cha utii kwa kamanda wa IS Abu Bakr al-Baghdad wiki tatu zilizopita. Aliongeza kwa kusema alitekeleza wito wa kiongozi huyo na namnukuu,waue makafiri nyumbani kwao na familia zao." amesema Molins.
Dola la Kiislamu IS limedai kuhusika na shambulio hilo la Jumatatu katika taarifa iliyorushwa na shirika la habari la Amaq ambalo hutoa matangazo ya kundi hilo mara kwa mara.
Polisi wanasema kwamba waliokota orodha katika eneo la tukio yenye majina ya polisi na wageni mashuhuri wakiwemo waandishi na wasanii kama walengwa wa mashambulizi. Pia waligundua visu vitatu kimoja kikiwa katika lindi la damu.
Tayari washirika watatu wa Abballa wamekamatwa wakihusishwa na shambulio hilo, mmoja wao aliwahi kutiwa hatiani mwaka 2013 kwa kujihusisha na mtandao wa kusajili wapiganaji wa jihadi nchini Pakistan.
Ulinzi waimarishwa
Wakati huo huo, polisi nchini Ufaransa wanazidi kuimarisha kikosi chao cha usalama kwa kupeleka askari zaidi kaskazini mwa nchi hiyo pamoja na kupanua marufuku ya pombe katika jitihada za kudhibiti vurugu zaidi kutokea katika mashindano ya soka barani Ulaya yanayoendelea nchini humo.
Mamlaka bado zina wasiwasi na mashabiki wa Urusi na wale wa Uingereza, waakti ambapo Uingereza itacheza dhidi ya Wales siku ya alhamis wakati Urusi ikimenyana na Slovakia.
Mjini Lille maduka yamelazimika kuacha kuuza pombe kwa saa zipatazo 60 kuanzia Jumanne hadi Ijumaa huku baa na migahawa ikitakiwa kufungwa usiku.
Zaidi ya wafanyakazi 2500 wa usalama wakiwemo askari polisi na wanajeshi wamemwagwa katika mji huo kama sehemu ya tahadhari ikiwa patatokea vurugu zingine.
Mwandishi:Sylvia Mwehozi/AFP/AP
Mhariri:Iddi Ssessanga