1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa yaimarisha usalama kufuatia mauaji ya Nice

Buwayhid, Yusra16 Julai 2016

Usalama umeimarishwa nchini Ufaransa baada ya mauaji ya lori ya mjini Nice, ambayo rais wa Ufaransa ameyataja ni ya kigaidi huku waendesha mashitaka wakisema, mshambuliaji hatambuliwi na vyombo vya usalama wa taifa.

https://p.dw.com/p/1JPt6
Frankreich Anschlag Soldaten
Picha: picture-alliance/AP Photo/C. Fahey

Usalama umezidi kuimarishwa nchini Ufaransa kwa kuongezwa vikosi vya akiba ikiwa ni pamoja na wanajeshi na maafisa wa polisi wa zamani 25,000. Mamlaka husika nchini humo zinajaribu kuchunguza sababu zilompelekea mshambuliaji, Mohamed Bouhlel ,raia wa Tunisia kuendesha lori katikati ya umati wa watu waliokuwa wakisherekea siku ya taifa la Ufaransa maarufu siku ya Bastile usiku wa kuamkia Ijumaa katika mji wa mwambao kusini mwa Ufaransa Nice. Shambulio lilosababisha vifo vya watu wasiopungua 84 na wengine 200 wakiwa wamejeruhiwa.

Miongoni mwa waliouawa ni wahamiaji na watalii kutoka mataifa mbalimbali ikiwa ni pamoja na Algeria, Tunisia, Ujerumani, Urusi, Ukraine, Uswisi, na Marekani na kumi kati yao ni watoto na miongoni mwa majeruhi 52 ni mahututi. Lori hilo lilitembea kwa zaidi ya kilomita mbili kabla ya polisi kumpiga risasi na kumuua Bouhlel. Kulingana na watu walioshuhudia, eneo la tukio Promenade des Anglais, lilifunikwa na maiti za watu.

Rais wa Ufaransa Francoise Hollande amerefusha muda wa hali ya hatari kwa miezi mitatu, na taifa hilo lipo katika hali ya maembolezo. Hollande pamoja na Waziri wake Mkuu Manuel Valls wameutaja kuwa ni uvamizi wa kigaidi lakini waendesha mashitaka wanasema Bouhlel, mwenye umri wa miaka 31 ambaye ni mkaazi wa mji wa Nice ,si mhalifu anayejulikana na vyombo vya usalama.

Frankreich Anschlag LKW rast in Nizza in Menschenmenge
Eneo la shambulio mjini NicePicha: Reuters/E. Gaillard

Bouhlel ni mhalifu uchwara

Hamna kundi lilojitokeza kuhusika na shambulio hilo hadi wakati huu. Naye waziri wa ndani, Bernard Cazeneuve, ametahadharisha kuwa ni mapema mno kuthibilisha kuwa ni shambulizi la kigaidi.

Mwendesha mashitaka wa Ufaransa, Francois Molins, amesema Bouhlel alikuwa amejaza silaha katika lori hilo alolikodi siku tatu kabla ya tukio, ikiwa ni pamoja na bunduki iliyojaa risasi silaha nyengine tatu pamoja na kombora lilokuwa tupu. Polisi walimdhania kuwa ni mhalifu uchwara anayetuhumiwa tokea mwaka 2010 kwa makosa ya wizi uharibifu wa mali za watu na ufanyaji vurugu. Molins amesema idara ya Ufaransa kuhusiana na habari za ujasusi haina taarifa zozote juu ya Bouhlel, na jina lake halikuwa katika orodha ya wahalifu walio na misimamo mikali.

Shambulio hilo la Nice limezua upya masuali yanayouliza kwanini Ufaransa imekuwa ikilengwa mfululizo kwa mashambulizi ya aina hii, na kipi kifanywe ili kuepusha matukio hayo?

Wapinzani wa kisiasa wa rais Hollande wameshaanza kunyoosha vidole vya shutuma, huku mgombea urais mtarajiwa, Alain Juppe, akisema mauaji ya Nice yangeweza kuepukika iwapo zingefuatwa hatua madhubuti za kiusalama.

Hollande ametangaza kuwa Ufaransa itaomboleza kwa siku tatu kuanzia Jumamosi, halikadhalika dakika moja ya ukimya itafanyika Jumatatu, kama sehemu ya kuwakumbuka waliouawa.

Kipindi cha hali ya hatari charefushwa

Ni shambulio la tatu katika kipindi kifupi cha miezi 18. Ufaransa iliomboleza vifo vya raia wake Januari 2015, pale wanajihadi waliposhambulia ofisi ya jarida la tashtit la kila wiki la Charlie Hebdo. Baadae lilifuatia mashambulio la risasi na pamoja na watu waliojito muhanga kwa kujilipua kwa mabomu mjini Paris November iliyopita ambapo watu 147 waliuawa.

Türkei Cumhuriyet Kolumne Charlie Hebdo
Jarida la Kila wiki la Ufaransa, Charlie HebdoPicha: Imago/ZUMA Press

Ufaransa ilitangaza kuwa katika hali ya hatari mwezi Novemba, lakini mauaji ya mjini Nice yameonyesha kuwa taifa hilo bado lipo katika hatari kubwa ya kufanyiwa mashambulizi.

Ndugu na jamaa walio nchini Tunisia katika mji wa Msaken alipotokea Bouhlel, wamesema wamestaajabishwa na wameaibishwa na tukio hilo la Nice. Serikali ya Tunisia imetoa taarifa rasmi ya kulaani shambulio la Nice na imesema itasaidiana na Ufaransa katika jitihada za kuwalinda raia na wakaazi wake. Viongozi wa mataifa mbalimbali pamoja na wanasiasa duniani kote wamelaani shambulio hilo la Nice nchini Ufaransa na kutuma salamu za rambirambi na mshikamano kwa Rais Hollande.

Ingawa hakuna kundi lilojitokeza kukubali kuhusika na mauaji ya Nice, Hollande ameapa kuwa Ufaransa itaimarisha mashambuliyi dhidi ya kundi linalojiita Dola la Kiisilamu IS nchini Syria na Iraq.

"Tutaendelea kuwashambulia wale wanaotuvamia katika ardhi yetu", amesema rais wa Ufaransa, Francois Hollande.

Kundi la IS limekua likiilenga Ufaransa kutokana na harakati zake za kijeshi dhidi ya kundi hilo nchini Iraq na Syria, na imeripotiwa kwamba mamia ya wanajihadi wametoka Ufaransa kwenda kujiunga na kundi la IS katika nchi hizo.

Mwandishi: Yusra Buwayhid

Mhariri: Sekione Kitojo