Ufaransa yaitisha mkutano kuhusu Syria
23 Novemba 2016Ufaransa sasa imeitisha mkutano wa nchi ambazo zinaunga mkono upinzani nchini Syria ikiwemo Marekani na mataifa ya ghuba kujadili hali ilivyo nchini humo hasa mashambulizi dhidi ya mji wa Aleppo. Hayo yanajiri wakati mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa Staffan de Mistura akihofia huenda rais Bashar al-Assad akafanya shambulizi baya zaidi kabla rais mteule Donald Trump kuapishwa.
Waziri wa mambo ya nje ya Ufaransa Jean-Marc Ayrault amesema mkutano huo wa nchi ambazo ni marafiki wa upinzani Syria utafanyika mjini Paris mapema mwezi Disemba. Amesisitiza kuwa jumuiya za kimataifa latiza zikome kuangalia tu uhalisia mchungu unaoendelea nchini Syria hasa mji unaoshambuliwa wa Aleppo.
Nchi ambazo zimealikwa ni pamoja na Marekani, Ujerumani, Italia, Uingereza na Uturuki, kando na mataifa ya ghuba hasa Saudi Arabia, Qatar, Jordan na Umoja wa Falme za Kiarabu. Jean Marc Ayrault anasema "Leo, karibu watu milioni moja wamezingirwa katika mashambulio kulingana na Umoja wa Mataifa, sit u Aleppo wala Homs lakini pia Ghouta na Idlib. Huo ndio uhalisia wa Syria kwa sasa. Ufaransa inachukua hatuaya mkutano kukabili mkakati huo wa vita unaofanywa na serikali na washirika wake ambao wamechukua nafasi ya ukosefu wa uhakika wa Marekani. Pia tutajadili msimamo wa Umoja wa Mataifa wa kukemea matumizi ya zana za kemikali na serikali ya Syria."
Raia washindwa kutoka maeneo ya vita
Takriban familia mia moja zilizojaribu kuhama mji huo usiku wa jana, zililazimika kurudi kufuatia mashambulizi makali yalizuka. hayo yamesemwa na kundi moja la uchunguzi. Serikali imeimarisha mashambulio kudhibiti mashariki ya mji huo ambao ni ngome kuu iliyosalia ya waasi, huku ikiwalaumu waasi kuzuia raia wasitoke na kuwatumia kama ngao. Madai ambayo waasi wameyakanusha na kuyataja kuwa uvumi.
Vikosi vya serikali ya Syria vinavyoungwa mkono na Urusi vimeendeleza mashambulizi makali dhidi ya mji wa Aleppo kuukumboa kutoka mikononi mwa waasi. Inakadiriwa kuwa raia 140 wamefariki katika kipindi cha wiki moja iliyopita kufuatia mashambulio hayo ya mabomu yanayorushwa na ndege za angani, vifaru na majeshi ya ardhini.
Hofu ya mashambulio zaidi
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Syria Staffan de Mistura amesema anayo hofu kwamba huenda rais Bashar al-Assad akafanya mashambulio mapya mashariki mwa Aleppo kabla ya rais mteule Donald Trump kuapishwa tarehe 20 Januari.
Japo de Mistura hajaelezea sababu ya hofu yake, wanadiplomasia wa Umoja wa Ulaya wamesema ushindi wa Trump umempa Assad matumaini ya ushirikiano na mshirika wake Urusi. Isitoshe anahisi serikali ya Obama huenda isijibu mashambulizi kama hayo ikizingatiwa imesalia na kipindi kifupi kuondoka madarakani.
Mwandishi: John Juma/RTRE/AFPE/
Mhariri: Josephat Charo