1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Onyo dhidi ya kuchapisha data zilizodukuliwa za Macron

6 Mei 2017

Ufaransa inachukuwa hatua kuzuwiya kudukuliwa kwa baruwa pepe za mgombea uchaguzi wa urais nchini Ufaransa Emmanuel Macron kushawishi matokeo ya uchaguzi huo kwa kuonya kwamba litakuwa kosa la jinai kuchapisha data hizo.

https://p.dw.com/p/2cX2R
Frankreich Wahl Emmanuel Macron Rede in Paris
Picha: Reuters/P. Wojazer

Ufaransa inachukuwa hatua kuzuwiya kudukuliwa kwa baruwa pepe za mgombea anayewekewa matumaini kushinda uchaguzi wa urais nchini Ufaransa Emmanuel Macron kushawishi matokeo ya uchaguzi huo kwa kuonya kwamba litakuwa kosa la jinai kuchapisha data hizo.

Timu ya Macron imesema udukuzi mkubwa umezitupa baruwa pepe, nyaraka na taarifa za kugharamia kampeni mtandaoni muda mfupi kabla ya kumalizika kampeni hapo Ijumaa na Ufaransa imeingia katika kipindi cha ukimya ambacho kinawapiga marufuku wanasiasa kuzungumzia juu ya kuvuja kwa nyaraka hizo.

Tume ya uchaguzi ya Ufaransa imesema katika repoti "Katika mkesha wa uchaguzi muhimu kabisa kwa taasisi zetu tume inatowa wito kwa kila mtu aliyeko kwenye mitandao ya kijamii hususan vyombo vya habari lakini pia raia kuonyesha kuwajibika kutosambaza maudhui hayo ili kutopotosha udhati wa uchaguzi."

Habari za kuvuja kwa data hizo zimeibuka wakati uchunguzi wa maoni ukionyesha Macron mgombea huyo yuko kwenye mkondo wa ushindi bila ya taabu dhidi ya kiongozi wa sera kali za mrengo wa kulia Marine Le Pen katika uchaguzi wa Jumapili ambapo uchunguzi wa mwisho ukionyesha kuongoza kwake kunaongezeka kwa kati ya asilimia 62 na 38.

Tume hiyo ambayo inasimamia mchakato wa uchaguzi imesema kufauatia mkutano wake ulioitishwa kwa haraka hapo Jumamosi kwamba data hizo zimepatikana kwa njia ya udanganyifu na zinaweza kuchanganywa na taarifa za uongo.

Agizo gumu kutekelezwa

Frankreich Marine Le Pen in Paris
Marine Le Pen kiongozi wa chama cha sera kali za mrengo wa kulia.Picha: picture-alliance/AP Photo/K. Zihnioglu

Hata hivyo agizo lake hilo inaweza gumu kulitekeleza katika eneo ambapo watu wanapata habari zao nyingi mtandaoni na habari hutiririka huru kwa kuvuka mpaka na watumiaji ni watu wasiojulikana.

Vyombo vya habari vya Ufaransa vimeshughulikia udukuzi huo kwa njia mbali mbali wakati chama mashuhuri cha sera za mrengo wa kushoto cha Liberation kimeupa umuhimu katika tovuti yake lakini habari katika vituo vya televisheni zimeamuwa kutoutaja.

Kama gigabytes 9 za data hapo Ijumaa usiku zimewekwa kwenye anuani ya mtandao inayoitwa EMILEAKS ukurasa wa mtandao wenye kuruhusu watu wasiojulikana kushirikiana matumizi ya nyaraka.

Bado haiko wazi nani aliyefanya hayo lakini vuguvugu la kisiasa la Macron limesema katika taarifa udukuzi huo ni jaribio la kuyumbisha demokrasia na kukiharibu chama hicho.Vuguvugu hilo la En Marche ikimaanisha kusonga mbele limesema limekuwa muhanga wa udukuzi mkubwa kabisa ulioratibiwa.

Kupotosha taarifa

Frankreich Whirlpool Streik Emmanuel Macon
Emmanuel Macon mgombea wa kujitegemea wa sera za mrengo wa kati.Picha: picture alliance/dpa/AP/T. Camus

En Marche imesema nyaraka zilizovuja zilikuwa zikihusu operesheni za kawaida za kampeni na zinajumuisha baadhi ya taarifa za mahesabu ya kampeni.Imesema wadukuzi wamechanganya nyaraka za uwongo na zile halisi "kuleta chokochoko ya mashaka na kupotosha taarifa."

Ufaransa ni taifa la hivi karibuni kabisa kuona uchaguzi mkubwa ukitiwa kiwingu na madai ya hila kupitia udukuzi wa mtandaoni baada ya mashirika ya ujasusi ya Marekani kusema hapo mwezi wa Januari kwamba Rais Vladimir Putin wa Urusi ameamuru kudukuliwa kwa vyama vyenye uhusiano na mgombea wa urais Hillary Clinton ili kuweka ushawishi wake katika uchaguzi huo kwa niaba ya mgombea wa chama cha Reublikan Donlad Trump.

Ikulu ya Urusi Kremlin imekanusha kuhusika na mashambulizi hayo ya udukuzi juu ya kwamba kambi ya Macron imeendelea kulalamika dhidi ya vyombo vya habari vya Urusi na kundi la wadukuzi lenye kuendesha shughuli zake nchini Ukraine.

Uchaguzi wa Jumapili unaonekana kuwa muhimu kabisa kwa Ufaransa kuwahi kushuhudiwa kwa miongo mingo ukiwa na maoni ya pande mbili yanayotafautiana kabisa kuhusu Ulaya na nafasi ya nchi hiyo katika jukwaa la dunia.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters

Mhariri :Zainab Aziz