1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa yaonya mataifa ya Ghuba dhidi ya kuiingilia Lebanon

8 Desemba 2017

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ayaonya mataifa yenye nguvu katika eneo la ghuba dhidi ya kuiingilia maswala ya Lebanon katika mkutano wa kimataifa uliolenga kuiondoa shinikizo utoka kwa wapinzani Iran na Saudi Arabia.

https://p.dw.com/p/2p2JD
Frankreich Paris Libanon Konferenz
Picha: Reuters/P. Wojazer

Akifungua mkutano huo, Macron alisema "ni muhimu kwa vyama vyote nchini Lebanon na mataifa yenye nguvu katika ukanda wa ghuba yakiwemo Saudi Arabia na Iran viheshimu kanuni ya msingi ya kutoingilia kati" mambo ya ndani ya nchi nyingine.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Rex Tillerson alihudhuria mazungumzo hayo mjini Paris na waziri mkuu wa Lebanon Saad Hariri, ambaye kujiuzulu kwake ghafla mwishoni mwa mwezi uliopita – kuliibua hofu ya kuzuka mgogoro mpya katika Mashariki ya Kati.

Wajumbe watano wa kudumu wa baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, pamoja na Ujerumani, Italia na Misri, waliwatuma wawakilishi kwenye mazungumzo hayo, ambayo yalikuwa yatazungumzia msaada wa kiuchumi na kibinadamu kwa taifa hilo lililotawaliwa na Ufaransa zamani.

Mazungumzo hayo yalifanyika wakati kukiwa na hali ya wasiwasi mkubwa Mashariki ya Kati iliyohusishwa na uamuzi wa Rais wa Marekani Donald Trump kuhamisha ubalozi wa Marekani huko Jerusalem, tangazo ambalo lilishtumiwa tena na Macron na Hariri.

Hariri alisema yafuatayo, "Inakwamisha mchakato wa amani hata zaidi (kati ya Israeli na Wapalestina) na inazusha changamoto mpya kwa usalama wa kikanda."     

Naye Macron aliongeza: "Hakuna matatizo yoyote ya kanda ambayo yatatatuliwa na maamuzi ya upande mmoja au mataifa yenye nguvu zaidi kuweka matakwa yao." 

 Saad Hariri, waziri mkuu wa Lebanon
Saad Hariri, waziri mkuu wa LebanonPicha: picture-alliance/AP Photo/T. Camus

Wakati huo huo Hariri ametoa wito wa msaada zaidi kutoka  jumuiya ya kimataifa kuisaidia nchi yake kukabiliana na wimbi la wakimbizi wa Syria.

Saudi Arabia na mataifa mengine ya Kiarabu yanailaumu Iran kwa kuyaunga mkono makundi yanayoendeleza migogoro kwa matumizi ya silaha kama vile Hezbollah ikiwa na lengo la kupanua ushawishi wake katika ukanda huo, kutoka Lebanon hadi Yemen, Syria na Iraq.

Hariri alibakia Riyadh kwa wiki mbili baada ya hotuba yake ya kujiuzulu, kukizuka uvumi kuwa alikuwa anazuiliwa kama mateka.

Macron aliingilia kati, akimwalika Hariri mjini Paris kwa ajili ya mazungumzo, baada ya hayo ambapo Hariri alirudi nyumbani akipewa makaribisho makubwa.

Baada ya kushauriana na vyama mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Hezbollah, Hariri alitangaza Jumanne iliyopita kwamba anafuta azma yake ya kutaka kujiuzulu.

Mwandishi. Fathiya Omar/ AFPE/APE

Mhariri:Yusuf Saumu