1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa yashambuliwa tena

Admin.WagnerD26 Juni 2015

Rais wa Ufaransa Francois Hollande amesema shambulio linalotuhumiwa kufanywa na mtu mwenye itikadi kali ya Kiislamu kwenye kiwanda cha gesi, ni la kigaidi Mtu mmoja alichinjwa na magaidi.

https://p.dw.com/p/1Fo73
Mashambulio mengine ya kigaidi nchini Ufaransa
Mashambulio mengine ya kigaidi nchini UfaransaPicha: Getty Images/AFP/P. Desmazes

Rais Hollande aliekuwa anahudhuria mkutano wa kilele wa viongozi wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels kuujadili mgogoro wa Ugiriki ,alirejea haraka nyumbani ili kuishughilikia kadhia hiyo. Rais huyo amesema mshambuliaji ameshatambuliwa na ameeleza huenda palikuwapo na mtu mwengine alieshiriki katika shambulio hilo.

Rais Hollande aliwaambia waandishi wa habari kwenye mkutano uliofanyika haraka, kwamba shambulio lilifanywa kutokea ndani ya gari iliyokuwa inaendeshwa na mtu mmoja au pengine alikuwapo mwengine.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo, watu waliiendesha gari hiyo kwa mwendo wa kasi sana na kuitosa katika kiwanda kilichokuwa na chupa za gesi. Rais Hollande ametamka kuwa lengo la watu hao bila shaka lilikuwa kusababisha mripuko. Hollande amesema shambulio hilo ni la kigaidi. Watu wengine kadhaa pia walijeruhiwa kutokana na shambulio hilo.

Waziri wa mambo ya ndani wa Ufaransa Benard Cazeneuve amewataka wananchi wa Ufaransa wasimame pamoja katika alichokiita kuwa ni mazingira magumu na pia amewahakikishia wananchi usalama wa hali ya juu. Waziri Cazeneuve pia ameelezea masikitiko juu ya mtu aliechinjwa.

Mtuhumiwa aliwahi kufanyiwa uchunguzi juu ya itikadi kali

Waziri wa mambo ya ndani wa Ufaransa Cazeneuve amearifu kwamba mtuhumiwa wa shambulio ambae amekamatwa aliwahi kufanyiwa uchunguzi miaka 9 iliyopita kutokana na tuhuma za kuhusika na itikadi kali.

Wakati huo huo mke wa mtu huyo pia amekamtwa. Ufaransa imekuwamo katika hali ya tahadhari tangu watu 12 wauliwe katika ofisi za jarida la vikatuni la Charlie Hebdo mnamo mwezi wa Januari.

,Viongozi wa nchi kadhaa barani Ulaya wamelilaani shambulio hilo lililofanywa na magaidi kwenye kiwanda kilichopo karibu na mji wa Lyon wa kusini magharibi mwa Ufarans Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron amesisitiza mshikamano na watu wa Ufaransa.

Uhispania na Ujerumani pia zimelilaani shambulio hilo la kigaidi.Waziri Mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy amesema katika mtandao wa Twitter kwamba unyama utakabiliwa na umoja miongoni mwa wapenda demokrasia.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank -Walter Steinmeier amesema nchi yake imesimama pamoja na Ufaransa. Waziri Steinmeier amesema ameshtushwa na mauaji ya kinyama.

Mwandishi:Mtullya Abdu./afp,rtre,

Mhariri: Iddi Ssessanga