Ufaransa yatangaza hati ya kukamatwa kwa Rais wa Syria Assad
15 Novemba 2023Hati hizo za kukamatwa ambazo zinahusu mashitaka ya kushirikiana katika uhalifu dhidi ya ubinadamu na kushirikiana katika uhalifu wa kivita, zinafuatia uchunguzi wa uhalifu katika mashambulizi ya kemikali katika mji wa Douma na wilaya ya Ghouta Mashariki mnamo Agosti 2013. Mashambulizi hayo yaliwauwa watu 1,000.
Ni waranti wa kwanza wa kimataifa kutolewa dhidi ya mkuu huyo wa nchi wa Syria. Kesi hiyo iliwasilishwa katika mahakama ya Ufaransa na Mazen Darwish, wakili na muasisi wa Kituo cha Habari na Uhuru wa Kujieleza cha Syria.
Syria inakanusha kutumia zana za sumu zilizopigwa marufuku lakini uchunguzi wa awali wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Shirika la Kuzuia Matumizi ya silaha za Kemikali ulipata kuwa serikali ya Syria ilitumia sumu ya kuua mishipa ya neva katika shambulizi lake la Aprili 2017 na imetumia mara kwa mara klorini kama silaha.