1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa yatishia kuishambulia Syria

14 Februari 2018

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron amesema Ufaransa itaanzisha mashambulizi iwapo itathibitika kama serikali ya Syria ilitumia silaha za sumu ambazo zimepigwa marufuku dhidi ya raia wake.

https://p.dw.com/p/2sekl
Präsident  Emmanuel Macron auf Korsica
Picha: Reuters/B. Tessier

Rais Macron aliiambia kurugenzi ya habari ya rais, "tutalishambulia eneo ambako mashambulizi haya yalifanywa ama eneo ambako yalikuwa yakipangwa. Lakini hadi leo bado hatujawa na uthibitisho kwamba silaha za sumu zilizozuiwa zimekuwa zikitumika dhidi ya raia'', aliongeza Macron na kuonya mara baada ya kuthibitisha kuwa atafanya kile alichokisema.

Alipoizungumzia serikali ya Syria, ama wakati au baada ya vita alisema "itawajibika yenyewe mbele ya mahakama ya kimataifa". Macron pia ametaka mkutano wa kimataifa juu ya Syria, kufanyika katika ukanda huo iwapo itawezekana.

Katika mawasiliano ya simu na Rais wa Urusi, Vladimir Putin Ijumaa iliyopita, Macron alisema alikuwa na mashaka kuhusu dalili zinazodhihirisha uwezekano kwamba silaha za sumu aina ya Chlorine zilitumika katika mashambulizi kadhaa dhidi ya raia nchini Syria katika wiki chache zilizopita.

Macron aliweka wazi itajibu kwa haraka matumizi ya silaha za sumu nchini Syria

Urusi imengilia mzozo huo, ikishirikiana na majeshi tiifu kwa serikali ya Syria katika vita vilivyodumu kwa miaka saba sasa, na Putin anaonekana kama kiongozi wa taifa la kigeni aliye na ushawishi mkubwa zaidi kwa Rais wa Syria, Bashar al-Assad.

Russland Sotschi Treffen Assad und Putin
Rais wa Syria Bashar al-Assad kushoto akiwa na rais wa Urusi Vladimir Putin kuliaPicha: Reuters/Sputnik/M. Klimentyev

Mnamo mwezi Mei, 2017 alipomkaribisha Putin katika kasri la Versaille, Macron aliweka wazi kwamba Ufaransa itajibu kwa haraka matumizi yoyote ya silaha za sumu nchini Syria.

Kulingana na Marekani, takriban mashambulizi sita ya silaha za sumu yameripotiwa tangu mapema Januari katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi, huku wengi wakijeruhiwa.

Serikali ya Syria, mwishoni mwa mwezi Januari ilikana kufanya mashambulizi ya silaha za sumu, na mshirika wake Urusi ikiyakanusha madai hayo na kuyaita kile ilichosema "kampeni za propaganda".

Kuna dalili zote zinazoonesha majeshi ya Syria yalitumia Chlorine

Wakati Ufaransa, kama ilivyo kwa Marekani, wakiituhumu serikali ya Syria, imesema bado haina vithibitisho madhubuti kuhusu asili na chanzo cha mashambulizi hayo. Jumatano iliyopita Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jeans-Yves Le Drian alisema kuna dalili zote zinazoonyesha kwamba majeshi ya serikali ya Assad yalitumia silaha za sumu ya Chlorine dhidi ya majeshi ya waasi, lakini akionyesha wasiwasi kwa kuwa bado hawana uhakika.

Syrien Bürgerkrieg Aleppo Luftangriffe
Wasyria wakimbilia maisha yao baada ya kusikia ndege ya kivita ikiangusha mabomuPicha: Reuters/M. Salman

"Katika hatua nyingine, shirika la habari la serikali ya Urusi RIA hii leo limenukuu duru kutoka wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo," alisema Le Drian, "zikisema taarifa zilizotolewa na vyombo vya habari kwamba mamia ya wanajeshi wa Urusi wamekufa wakati wakipambana katika vita nchini Syria ni za "upotoshaji wa hali ya juu," aliongeza afisa huyo wa Ufaransa.

Washirika wa jeshi la Urusi wanaopigana kwa ushirikiano na jeshi la serikali ya Syria, wamesema kulikuwa na idadi kubwa ya majeruhi miongoni mwa wanajeshi hao, wakati vikosi vya muungano vinavyoongozwa na Marekani vilipokabiliana na majeshi tiifu kwa serikali ya Syria katika jimbo la Deir al-Zor Februari 7.

Taarifa nyingine kutoka nchini Syria zinasema, Rais Assad na washirika wake wanakaribia ushindi wa mwisho katika mapambano dhidi ya kundi la wanamgambo linalojiita Dola la Kiislamu, IS. Kumeanzishwa mashambulizi mapya, ambayo yanatishia mzozo mbaya miongoni mwa nchi zenye nguvu duniani na kwenye ukanda huo.

Mwandishi: Lilian Mtono/rtre/ape/afpe

Mhariri: Grace Patricia Kabogo