Ufaransa yatowa ripoti mauaji ya Rwanda
26 Machi 2021Kiongozi wa tume hiyo, mwanahistoria Vincent Duclert alitarajiwa kuikabidhisha ripoti hiyo kwa Macron jioni ya Ijumaa (Machi 26) kabla ya kuwekwa hadharani, kwa mujibu wa taarifa ya ofisi ya rais.
Inadaiwa kwamba Ufaransa, wakati huo ikiongozwa na Rais Francois Mitterand, haikufanya jitihada za kutosha kuzuwia mauaji ya maangimizo dhidi ya watu 800,000, wengi wao kutoka jamii ya wachache ya Watutsi, na kwamba hata ilikuwa sehemu ya uhalifu huo.
Suala hili bado linayaathiri sana mahusiano baina ya nchi hizo mbili kwa takribani robo karne tangu Paul Kagame, ambaye mwenyewe anatokea kabila la Kitutsi, atawale Rwanda baada ya mauaji hayo.
Macron aliamuru kuundwa kwa tume hiyo mwezi Mei 2019 kuchambuwa dhima ya Ufaransa nchini Rwanda kutoka mwaka 1990 hadi 1994 kwa kutumia utafiti wa makumbusho.
Jinsi mauaji yalivyoanza
Mauaji hayo ya kimbari yalianza baada ya Rais Juvenal Habyarimana, ambaye alikuwa Mhutu na aliyekuwa na mahusiano makubwa na Ufaransa, kufariki dunia pale ndege yake ilipoangushwa katika anga ya Kigali, mnamo tarehe 6 Aprili 1994.
Ufaransa ilikuwa ikiongoza operesheni ya kijeshi na kibinaadamu chini ya idhini ya Umoja wa Mataifa kati ya mwezi Juni na Agosti 1994.
Wakosoaji wake wanaamini Ufaransa ilikuwa hasa inatumia operesheni huyo kuisaidia serikali iliyokuwa ikiongozwa na Wahutu.
Kumekuwepo pia tuhuma za mara kwa mara kwamba mamlaka nchini Ufaransa ziliwasaidia washukiwa wa mauaji hayo ya kimbari nchini Rwanda kukimbia nchi huku wakilindwa na jeshi la Ufaransa.
Kazi ya Tume ya Duclert
Hata hivyo, tume hiyo yenye wajumbe 15 haina hata mtaalamu mmoja wa masuala ya Rwanda, jambo ambalo ofisi ya rais wa Ufaransa inasema ilikuwa muhimu kuhakikisha hakuna upendeleo wowote.
Lakini wanahistoria hao - wanaojumuisha wataalamu wa mauaji ya maangamizo dhidi ya Mayahudi na Waarmenia kwenye Vita vya Kwanza vya Dunia na pia wa sheria za kimataifa - wamefanikiwa kuzipata nyaraka kadhaa zikiwemo za mwenyewe Rais Mitterrand ambazo kwa muda mrefu zilikuwa zimezuiliwa kuonekana na watafiti.
Vile vile wamezipitia nyaraka za waziri mkuu wa zamani kutoka mrengo wa siasa kali za kulia, Edouard Balladur, ambaye wakati wa mauaji hayo alikuwa ndiye kiongozi wa baraza la mawaziri. Walipitia pia nyaraka za wizara za ulinzi, mambo ya nje na idara ya ujasusi wa nje, DGSE.
Duclert mwenyewe alikwenda Rwanda mwezi Februari 2020 lakini kumekuwa na wasiwasi juu ya uhuru wa tume yake, hasa kwa kuwa imekuwa ikifanya kazi nje ya wizara ya ulinzi mjini Paris.