1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa yaweza kurejesha kodi wanayotozwa matajiri

Daniel Gakuba
5 Desemba 2018

Ufaransa imesema inatathmini kurejesha kodi kwa wenye kipato kikubwa, ambayo ilifutwa na Rais wa nchi hiyo Emmanuel Macron baada ya kuingia madarakani. Hilo ni moja ya madai makuu katika maandamano ya hivi karibuni.

https://p.dw.com/p/39Ur8
Frankreich Präsident Emmanuel Macron bei Paris auto show
Rais wa Ufaransa, Emmanuel MacronPicha: Reuters/R. Duvignau

 

Uwezekano wa kurejeshwa kwa kodi hiyo maarufu kama ISF iliyokuwa ikitozwa kwa wenye kipato kikubwa nchini Ufaransa umetajwa na msemaji wa serikali ya nchi hiyo Benjamin Griveaux katika mahojiano na kituo cha redio cha RTL. Ingawa msemaji huyo amesema uamuzi kuhusu hatua hiyo haujawekwa kwenye meza ya mazungumzo, ikiwa sera fulani haileti ufanisi, serikali sio kiziwi, italibadilisha.

Kufuta kodi hiyo ilikuwa ahadi muhimu ya kampeni ya urais ya Emmanuel Macron anayependelea biashara, kama njia ya kurahisisha uwekezaji na kuundwa kwa nafasi za ajira.

''Rais wa matajiri, asiyewajali maskini''

Lakini wakosoaji wake, wakiwemo wengi walioshiriki katika maandamano yenye fujo yaliyoandaliwa siku za hivi karibuni na vuguvugu la vizibao vya njano katika maeneo mengi ya nchi, wamekuwa wakichukizwa na mtazamo wa rais Macron, wakimshutumu kuwapuuza wanyonge, kama alivyolalamika mwandamanaji huu ambaye ni mwanamme wa makamo.

Gilets jaunes Proteste gegen Erhöhung der Benzinpreise in Frankreich
Maandamano ya vuguvugu la vizibao vya njano yameitikisa Ufaransa siku za hivi karibuniPicha: AFP/Getty Images/F. Guillot

''Ninavyodhani mimi, chanzo cha matatizo yote ni kwamba bwana Macron anawapenda matajiri, anawapenda wenye nguvu, anawahusudu mabosi wakubwa katika taasisi za kifedha. Anapenda matajiri kama alivyosema Hollande, na hawajali watu wa kawaida. Na sio kwamba hawajali tu, bali pia anawadharau, na sababu hiyo ndio imetufikisha hapa.'' Amesema mwandamanaji huyo.

Vuguvugu la Vizibao vya njano ambalo lilianzia kwenye jukwaa la kupinga kodi kwenye mafuta ya dizeli iliyopandisha bei ya bidhaa hiyo inayotegemewa na wengi, lilikua na kugeuka malalamiko mapana dhidi ya kupanda kwa gharama ya maisha, na hasira dhidi ya sera za rais Macron alichukuliwa na wengi kuyafumbia macho masaibu ya watu wa vijijini na miji midogo nchini Ufaransa.

Umaarufu wa Macron waporomoka

Hapo jana, waziri mkuu wa Ufaransa Edouard Philippe aliahirisha kwa miezi sita kodi hiyo kwa mafuta ya dizeli, muda ambao alisema utatumiwa kushauriana na wote wanaoathiriwa na kodi hiyo. Msemaji wa serikali Griveaux amesema ikiwa hakuna makubaliano yatakayopatikana, basi kodi hiyo kwa mafuta ya diseli itafutwa kabisa.

Uungwaji mkono wa Rais Emmanuel Macron mwenye umri wa miaka 40 umeporomoka miongoni mwa wapiga kura, ambapo uchunguzi mpya wa maoni unaonyesha kuwa Wafaransa 24 asilimia ndio wanaoridhishwa na kazi anayoifanya.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe, rtre

Mhariri: Iddi Ssessanga