Ufilipino yaamuru kukamatwa tena kwa mshukiwa wa mauaji
16 Julai 2023Mahakama kuu ya Ufilipino imeamuru kukamatwa tena kwa mwanasiasa wa zamani anayetuhumiwa kumuua mwanamazingira mashuhuri, zaidi ya muongo mmoja uliopita. Haya ni kwa mujibu wa nyaraka za mahakama zilizochapishwa leo.
Joel Reyes, gavana wa zamani wa kisiwa cha magharibi cha Palawan, ameshutumiwa kwa kupanga mauaji ya 2011 ya Gerry Ortega, ambaye alitumia kipindi cha redio alichokuwa akikiandaa mara kwa mara kumshutumu Reyes kwa ufisadi unaohusishwa na uhalifu wa mazingira katika kisiwa hicho.
Soma pia: Ufilipino: Gavana na watu wengine 5 wauawa kwa kuyatuliwa risasi
Ortega aliuawa kwa kupigwa risasi alipokuwa akifanya manunuzi katika mji mkuu wa Palawan, mojawapo ya visiwa vikubwa nchini humo na kivutio maarufu cha watalii kwa misitu yake mikubwa na mandhari safi.
Reyes na kaka yake Mario, ambaye pia alihusishwa na mauaji ya Ortega, walitoweka mwaka 2012 baada ya tangazo la kutafutwa kwao kutolewa. Walikamatwa nchini Thailand mnamo 2015.
Reyes aliachiliwa kutoka jela mwaka wa 2018 baada ya mahakama kutupilia mbali mashtaka ya uhalifu dhidi yake. Mawakili wa serikali, hata hivyo, walikata rufaa dhidi ya uamuzi huo na mashtaka yakarejeshwa karibu miaka miwili baadaye.