Uganda kuwaomba wakopeshaji kuchelewesha ulipaji madeni
26 Aprili 2021Nia hiyo ya serikali ya Uganda imetangazwa na waziri wa fedha wa taifa hilo Matia Kasaija ambaye amesema wanaweza kuwaomba wakopeshaji wasitishe kwa hadi miaka miwili ulipaji wa madeni kuruhusu nchi hiyo kujiweka sawa kiuchumi.
Haya yametanagzwa wakati wasiwasi ni mkubwa kuwa taifa hilo huenda likashindwa kulipa mzigo mkubwa wa fedha ilizokopa kutoka nje.
Mwaka uliopita taifa hilo la Afrika Mashariki lilichukua kiwango kikubwa cha mikopo kutoka Benki ya Dunia, Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF, na wakopeshaji wengine kukabiliana na msukosuko wa kiuchumi uliosababishwa na janga la virusi vya corona.
Mikopo hiyo imeongeza mzigo mwingine kwenye deni la taifa ambalo tayari ni kubwa na linazitia mashaka baadhi ya taasisi ikiwemo Benki Kuu ya nchi hiyo na shirika la Fedha la IMF.
Deni la Taifa laongezeka kwa asilimia 35 mwaka 2020
Hadi Disemba mwaka jana deni jumla la taifa nchini Uganda lilipanda kwa dola bilioni 18 za Marekani,kiwango ambacho ni sawa na ongezeko la asilimia 35 ikilinganishwa na mwaka uliopita.
Hali hiyo ilichochewa na uamuzi wa seirkali ya Uganda kuchukua mikopo mipya kufidia nakisi ya bajeti iliyosababishwa na kuanguka kwa mapato ya ndani kulikochangiwa na kudodora kwa uchumi na mifumo dhaifu ya ukusanyaji wa kodi.
Data za wizara ya fedha zinaonesha zaidi ya theluthi mbili ya deni jumla la Uganda ni kutoka wakopeshaji wa nje.
Kulingana na waziri wa fedha wa Uganda Matia Kasaija katika mwaka wa fedha unaomalizika mwezi Juni 2021, deni la taifa la nchi hiyo litapindukia asilimia 50 ya pato jumla la ndani kiwango ambacho kinatia mashaka.
Waziri Kasaija ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa hali hiyo haileti faraja ikizingatiwa kuwa Uganda italazimika kutumia asilimia 20 ya mapato yote ya mwaka wa fedha unaokuja ili kulipa madeni.
Uganda inachechemea kama mataifa mengine kadhaa ya Afrika
Uganda inajiunga na mataifa mengine ya Afrika ikiwemo Ethiopia, Zambia na Chad ambayo yanaandamwa na mzigo mkubwa wa madeni na inayawia vigumu kuyalipa kufuatia kuanguka kwa shughuli za uchumi tangu kuzuka kwa janga la corona.
Uchumi wa Uganda uliporomoka kwa hadi asilimia 1.1 mwaka uliopita lakini unatazamiwa kufikia ukuaji wa asilimia 3.1 mwaka 2021.
Uganda ilikuwa miongoni mwa mataifa yaliyonufaika kwa sehemu kubwa na mpango wa Benki ya Dunia na shirika la Fedha la IMF wa kuyafutia madeni mataifa masikini yaliyoelemewa mwanzoni mwa miaka ya 2000.
Hata hivyo miongo kadhaa baadaye serikali ya rais Yoweri Museveni ilianza tena kukopa kwa wingi hususani kutoka China ili kufadhili miradi mikubwa ya miundombinu ikiwemo barabara, viwanja vya ndege na vituo vya kufua umeme vilivyogharimu mabilioni ya dola.