1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugiriki: Tsipras arudi kwa kishindo

21 Septemba 2015

Alexis Tsipras, kiongozi wa Ugiriki mwenye sera za mrengo wa kushoto, amerejea madarakani kwa kishindo, baada ya chama chake cha Syriza kupata ushindi ambao haukutarajiwa katika uchaguzi mkuu uliofanyika jana Jumapili.

https://p.dw.com/p/1GZZo
Alexis Tsipras baada ya ushindi unaomrejesha kwenye kilele cha siasa za Ugiriki
Alexis Tsipras baada ya ushindi unaomrejesha kwenye kilele cha siasa za UgirikiPicha: Reuters/A. Konstantinidis

Baada ya kuhesabiwa asilimia zaidi ya 99 ya kura zote zilizopigwa, matokeo yanaonyesha chama cha Syriza kikiongoza kwa asilimia 35.5, kikifuatiwa na chama cha kihafidhina cha New Democracy kilichopata asilimia 28.1. Ushirikiano kati ya chama cha Syriza na chama mshirika cha Independent Greeks una jumla ya viti 155 katika bunge la Ugiriki lenye viti 300, idadi ambayo inatosha kuunda serikali.

Akiwahutupia wafuasi wake waliojawa na furaha baada ya ushindi, Tsipras hakughusia mkopo wa euro bilioni 86 unaolemea mabega ya nchi yake, lakini amedokeza kuhusu kazi kubwa iliyo mbele yake.

''Tuna changamoto mbele yetu, lakini pia tunao msingi imara, tunajua ni wapi tunaweza kukanyaga, na tunayo matumaini. Jawabu la mgogoro wa kiuchumi unaotukabili halitapatikana kimiujiza, bali litapatikana kupitia kazi ngumu''. Amesema Tsipras.

Ridhaa ya kushika hatamu

Ushindi huu unamhakikishia kiongozi huyo nafasi ya kuendelea kuidhibiti siasa ya nchi yake, licha ya kutupwa mkono na wahafidhina ndani ya chama chake mwezi uliopita, kufuatia uamuzi wake kuridhia masharti ya wakopeshaji, ambayo yanaambatana na hatua kali za kubana matumizi.

Kiongozi wa chama cha New Democracy, Evangelos Meimarakis amekubali kushindwa
Kiongozi wa chama cha New Democracy, Evangelos Meimarakis amekubali kushindwaPicha: dapd

Huu ulikuwa uchaguzi mkuu wa tano katika muda wa miaka sita nchini Ugiriki. Tsipras amewaahidi wafuasi wake kipindi cha utengamano kisiasa, akisema sasa atautumikia mhula wake kamili wa miaka minne.

Kazi kubwa ya kwanza kwenye ya bwana Alexis Tsipras itakuwa kuunda serikali ambayo itawashawishi wakopeshaji ndani ya Umoja wa Ulaya, kwamba juhudi za kutosha zimechukuliwa kuruhusu kutolewa kwa awamu nyingine ya mkopo. Tarehe ya kuutathimini mkopo huo itawadia mnamo mwezi ujao.

´Wakopeshaji wafuatilia kwa karibu

Tayari mwenyekiti wa baraza la mawaziri wa fedha wa nchi zinazotumia sarafu ya Euro, Jeroen Dijsselbloem amekwishatoa kauli, kuhusu matumaini waliyo nayo kufanya kazi na serikali mpya ya Ugiriki.

Haitakuwa kazi rahisi kwa Tsipras kuridhisha matumaini ya wagiriki wanaoteswa na kuanguka kwa uchumi wa nchi yao
Haitakuwa kazi rahisi kwa Tsipras kuridhisha matumaini ya wagiriki wanaoteswa na kuanguka kwa uchumi wa nchi yaoPicha: Reuters/A. Konstantinidis

Kupitia ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa Twitter, Dijsselbloem amesema, ''Tuko tayari kushirikiana na serikali ya Ugiriki, na kuendelea kuisindikiza nchi hiyo katika juhudi zake kubwa za mageuzi''.

Hata hivyo, katika kile kinachochukuliwa na wachambuzi kuwa ishara ya manung'uniko miongoni mwa wananchi, uitikiaji wa uchaguzi huo ulikuwa wa kiwango cha chini. Zaidi wa asilimia 40 ya wapiga kura hawakuona haja ya kwenda kwenye vituo vya kupiga kura, na asilimia 7 ya waliojitokeza wamekichagua chama cha Golden Dawn, au Mapambazuko ya Dhahabu, ambacho kiliundwa na vuguvugu lenye mtazamo wa kinazi mamboleo.

Mwezi uliopita, Alexis Tsipras alijiuzulu wadhifa wa waziri mkuu, baada ya mpasuko ndani ya chama chake, kutoka na kukubali kwake masharti ya wakopeshaji, ambayo alikuwa amechaguliwa chini ya kauli mbiu ya kuyakataa.

Mwandishi: Daniel Gakuba/ape/rtre

Mhariri: Iddi Ssessanga