1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugonjwa wa Corona waripotiwa mashariki ya kati

Saleh Mwanamilongo
24 Februari 2020

Kuwait na Bahrain zimethibitisha visa vya kwanza vya Corona. Irak ilithibitisha pia kisa kimoja cha Corona kwenye ardhi yake,mjini Najaf.Afghanistan na Oman pia zimetangaza visa vya kwanza vya ugonjwa huo.

https://p.dw.com/p/3YKFT
Raia wahofia kuambukizwa virusi vya Corona ,jijini Teheran, Iran
Raia wahofia kuambukizwa virusi vya Corona ,jijini Teheran, IranPicha: picture-alliance/ZUMAPRESS.com/R. Fouladi

Viongozi wa serikali ya Iran wameahaidi kuwepo na uwazi kuhusu ugonjwa wa Corona nchini humo, huku wakikanusha vikali madai kwamba idadi ya vifo vilivyotokana na mripuko huo ni watu 50. Wakati huohuo Italia inajaribu kuzuwia ugonjwa huo kuenea nchi jirani baada ya vifo 5 kuthibitishwa kaskazini mwa nchi hiyo.  Italia inaaminika hivi sasa kuwa kitovu cha ugonjwa wa Corona barani Ulaya. 

Naibu waziri wa afya nchini Iran, Iraj Harirtchi amekanusha taarifa kwamba watu 50 tayari wamekufa na ugonjwa wa Corona nchini humo. Ahmad Amirabadi Farahani, mbunge wa jimbo la Qom, ambako kulitangazwa visa vya kwanza vya ugonjwa huo nchini Iran, amesema kwamba idadi ya vifo ilifikia takriban watu 50 kwenye mji huo mtakatifu wa wa shia, ulioko umbali wa kilometa 150 kusini mwa mji mkuu Tehran.

Naibu waziri wa afya, alisema kwamba ni uongo mtupu. '' Nimemuomba ndugu yetu alietoa idadi hiyo ya vifo vya watu 50,atupe daftari ya majina yao. Na ikiwa idadi ya vifo inafikia nusu au robo ya idadi alioitowa basi nitajiuzulu,'' amesema naibu waziri huyo wa afya.

"Tunaahidi kuwa wawazi kuhusu kutangaza idadi ya visa vya Corona," alisema kwa upande wake  msemaji wa serikali, Ali Rabii. "Tutatangaza idadi zote za vifo nchini kote," aliendelea kusema.

Shirika la habari la Ilna, mjini Teheran lilielezea kwamba, haliwezi kuzuia taarifa yeyote inayohusiana na ugonjwa huo wa Corona,huku likimnukuu mbunge Farahani akisema kwamba ''serikali haiwambie ukweli raia wake''.

Viongozi walitangaza idadi mpya ya watu 4 waliofariki siku ya Jumatatu na kufikia watu 12 waliofariki nchini humo miongoni mwa watu 61 walioambukizwa na Corona kwa mujibu wa wizara ya afya ya Iran.

Polisi akivaa kifaa cha kujikinga kwenye carnivali ya mjini Venice, Italia
Polisi akivaa kifaa cha kujikinga kwenye carnivali ya mjini Venice, Italia Picha: Reuters/M. Silvestri

Idadi hiyo imeiweka Iran kuwa nchi ilioathirika zaidi kufikia sasa na ugonjwa wa Corona, baada ya China ambako watu zaidi ya 2,600 wamekufa.

 Visa kadhaa zaidi kwenye nchi za mashariki ya kati

Nchi zingine mfano wa Kuwait, Bahrain, zimethibitisha visa vya kwanza vya Corona, vilivyoingizwa na wasafiri kutoka Iran.

Kwa upande wake Irak ilithibitisha pia kisa kimoja cha Corona kwenye ardhi yake, kutoka kwa mwanafunzi wa dini kutoka Iran ambae alithibitishwa kuwa na kirusi cha Corona mjini Najaf. Afghanistan na Oman pia zimetangaza visa vya kwanza vya ugonjwa huo.

Nchini Italia, viongozi wametangaza kuzidisha uchunguzi wa kiafya ili kuutokomeza ugonjwa wa Corona. Miji 12 tayari imewekwa kwenye karatini  kaskazini mwa nchi hiyo ilikuzuia kuenea kwa ugonjwa huo katika nchi jirani za Ulaya.

Idadai ya watu walioambukizwa na virusi vya Corona ilipanda kutoka watu sita hadi 219 mnamo kipindi cha siku nne pekee.