1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uharamia biashara katika Pembe ya Afrika

J.Scholz - (P.Martin)2 Desemba 2008

Maharamia wa Kisomali wamejiandaa vizuri na wana silaha za kisasa kabisa.Vitendo vyao vya haramu vimekuwa njia ya kujipatia idadi kubwa sana ya fedha katika Pembe ya Afrika.

https://p.dw.com/p/G7XU

Mashambulizi ya maharamia hao sasa ni kitisho kikubwa kwa ulimwengu mzima.Mwezi huu serikali ya Ujerumani itaamua kwa umbali gani ishiriki katika ujumbe wa Umoja wa Ulaya kupiga vita uharamia.Kwa maoni ya Jeshi la Ujerumani Bundeswehr,kundi la manowari 500 za kijeshi zinahitajiwa ili ujumbe wao uweze kufanikiwa katika Pembe ya Afrika kwani maharamia wana silaha za kisasa na wamejitayarisha vizuri.Kwa mfano hivi sasa maharamia wamewazuia mateka mabaharia 250 na kama meli 12.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Kimataifa ya Misafara ya Meli mjini London,mwaka huu peke yake maharamia wamefanya mashambulizi 92 katika eneo la Pembe ya Afrika.Kwa wastani fedha zinazodaiwa kukomboa kila meli moja ni kati ya dola milioni moja hadi mbili isipokuwa kwa meli ya Saudi Arabia iliyobeba mafuta.Hapo maharamia wamedai dola milioni 25. Vyombo vya habari vya kanda hiyo vinasema kuwa kawaida fedha za kukomboa meli na wafanyakazi wake hupelekwa moja kwa moja kwenye meli yenyewe.Lakini nani anenufaika kutokana na pesa hizo?Mtaalamu wa masuala ya Somalia Roger Middleton alipozungumza kutoka makao ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa mjini London alisema:

"Wengi wao wanafuata maslahi yao na huteka nyara meli yo yote inayopita njia,lakini kwa hakika makundi hayo ya maharamia yana mawasiliano na nchi zingine.Baadhi ya maharamia husema waziwazi kuwa wana washirika wao katika Mashariki ya Kati,Ulaya na Amerika."

Bila shaka uharamia ni matokeo ya kutokuwepo serikali inayofanya kazi nchini Somalia tangu mwaka 1991.Serikali ya mpito inayoongozwa na Rais Abdullahi Yusuf Ahmed kwa mara ya kumi na tano inajaribu kupata suluhisho la amani.Nchini humo,hakuna serikali wala sheria zinazofanya kazi.Mwa mujibu wa mashirika yanayotoa misaada ya kiutu,nusu ya Wasomali wanategemea msaada kutoka nchi za kigeni na miongoni mwao kuna maelfu wanaoteseka kwa njaa.

Umasikini mkubwa,biashara ya magendo inayoshamiri pamoja na maafisa wa serikali wanaohusika na rushwa ni hali zinazotoa nafasi nzuri kwa maharamia kulitumia eneo hilo la Somalia kwa vitendo vyao vya uhalifu.

Middleton akieleza juu ya matukio ya hivi sasa katika Pembe ya Afrika anasema:

"Lazima itambuliwe kuwa tatizo la uharamia linalotusumbia sote hivi sasa ni matokeo ya kutokuwepo na serikali inayofanya kazi nchini Somalia na hali hiyo imesababishwa na mambo mengi."

Kwa maoni ya Middleton,sababu mojawapo ni kwamba jumuiya ya kimataifa haikutia sana maanani matatizo ya nchini Somalia.Ikiwa jumuiya ya kimataifa kweli inataka kukomesha uharamia basi matatizo ya kisiasa ya Somalia yanapaswa kupatiwa ufumbuzi.Hiyo ni njia pekee ya kupata suluhisho la kudumu kwa tatizo la uharamia kwenye Pembe ya Afrika.