Uholanzi yaibwaga Chile, Uhispania yajiliwaza na Australia
24 Juni 2014Mchuano kati ya Uholanzi na Chile ulianza kwa kasi, lakini bila ya ubunifu katika safu ya mashambulizi jinsi ilivyodhihirika kwa kubakia sifuri kwa sifuri kwa kipindi kirefu cha mchezo.
Chile ilianza kama timu yenye mashambulizi makali wakati Uholanzi ikicheza kwa tahadhari wakilenga kuwapiga wapinzani wao kwa mfumo wa counter attack. Kiungo nyota wa Chile Arturo Vidal alikuwa kwenye benchi baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti mwezi uliopita, jambo ambalo liliwakosesha Chile ubunifu uwanjani.
Nyota wa Barcelona Alexis Sanchez alikuwa tishio kubwa kwa upande wa Wachile, huku akiisumbua safu ya ulinzi ya Uholanzi.
Ilikuwa katika dakika ya 77 wakati Leroy Fer wa klabu ya Norwich City ya Uingereza, dakika mbili tu baada ya kuingia kama nguvu mpya, akafunga goli kwa njia ya kichwa baada ya kuandaliwa krosi safi na Daryl Janmaat.
Memphis Depay alifanya mambo kuwa mawili kwa sifuri baada ya mchezaji wa Bayern Munich Arjen robben kutimka kama umeme na kumsukumia mpira kiungo huyo wa PSV ambaye naye akamalizia hadi wavuni.
Australia, Uhispania wacheza kwa ajili ya sifa tu
Katika mchuano mwingine wa Kundi B, baina ya Australia na Uhispania, ambapo mabingwa hao – wakiwa tayari wameondolewa kwenye dimba hilo – waliepuka fedheha ya kutopata points zozote katika awamu ya Makundi.
Fernando Torres alifunga goli baada ya kuunganisha pasi ya Iniesta na kufany amabao ya Uhispania kuwa mawili kwa sifuri. Australia walianza kwa kasi, lakini labda kutokana na kukosekana uwanjani kwa mchezaji wao gwiji Tim Cahill, ambaye anatumikia adhabu ya kadi nyingi za njano, walishindwa kuonyesha mashambulizi makali waliyokuwa wakifanya katika mechi za awali.
Wakati Uhispania walipoanza kupata udhibiti wa mchezo, David Villa alionekana kuwa mwiba katika ngome ya Socceroos. Goli la kwanza la Uhispania likuwa katika dakika ya 36 wakati Villa – ambaye alikuwa akicheza mchuano wake wa mwisho na timu ya taifa – alipofunga goli kwa kisigino kutokana na krosi ya Juanfran.
La pili lilikuja katika dakika ya 69 wakati Iniesta alipoandaa pasi safi kabla ya Fernando Torres kumalizia wavuni. Katika dakika ya 82 masaibu ya Australia yaliongezeka wakati Cesc Fabregas alipouinua mpira juu ya walinzi wa Australia, na kumpa Juan Mata muda wa kutosha kuusukuma mpira katikati ya miguu ya kipa Mathew Ryan hadi ndani ya nyavu.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Sekione Kitojo