1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhuru atangaza sheria za corona eneo la Ziwa na Bonde la Ufa

Josephat Charo
29 Juni 2021

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ametangaza sheria mpya za kupambana na ugonjwa wa COVID 19 katika eneo la kanda ya Ziwa na Bonde la Ufa.

https://p.dw.com/p/3vltM
Kenia Coronavirus Uhuru Kenyatta
Picha: PSCU

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alisema kuanzia Jumanne (29.06.2021) muda wa kutotoka nje usiku saa moja utaendelea kudumishwa hadi tarehe 31 mwezi wa Julai 2021. Maeneo mengine ya nchi ambako muda huo huanza saa nne usiku hadi saa kumi alfajiri yataendelea na utaratibu huo kwa siku 60 zijazo.

Idadi ya wanaohudhuria ibada iko pale pale kuwa ni thuluthi moja ya watu wote.

Uhuru aliongeza kusema kuwa wageni wote wanaoingia ndani ya mipaka ya Kenya sharti wawe na cheti cha vipimo ambavyo vimefanywa saa 96 kabla kusafiri. Maziko na misiba kufanyika katika muda wa saa 96 na kuwashirikisha watu wasiozidi 100 kadhalika harusi.

Uhuru alisema kuhusu mipango ya muda mrefu ya kupambana na COVID 19, serikali ya Kenya inajiandaa kuagiza kutoka nje viungo vya chanjo badala ya dozi kamili. Ifikapo Disemba mwakani,watu milioni 10 watakuwa wamepata chanjo ya COVID 19.

Mipango ya baadaye inajumuisha pia kuunda kiwanda maalum cha kutengeza chanjo za binadamu na wanyama zitakazosambazwa kwenye kanda ya Afrika Mashariki hadi eneo la kaskazini na Morocco.

Ipo haja ya taasisi za dini na jamii kuuelimisha umma kuhusu manufaa ya chanjo ya COVID 19 ili kuzuwia maambukizi na kuimarisha kinga ya mwili, alieleza Rais Uhuru Kenyatta.

Na Thelma Mwadzaya