Uhuru wa kujieleza: DW yawatuza waandishi
3 Mei 2020Waliotuzwa waliipokea tuzo hiyo kwa niaba ya waandishi wote wa habari duniani wanaochapisha taarifa kuhusiana na janga la corona huku wakifanya kazi katika mazingira magumu.
"Katika kipindi cha dharura ya afya kote duniani, uandishi wa habari una jukumu muhimu na kila mwandishi ana jukumu kubwa sana," alisema Mkurugenzi Mkuu wa DW Peter Limbourg wakati akiwatangaza washindi mjini Berlin.
"Raia wa nchi yoyote wana haki ya kupata taarifa inayotokana na ukweli na uchunguzi wa kina," alisema Limbourg. "Udhibiti wa kinachoandikwa huenda ukasababisha hali mbaya na jaribio lolote la kuwafanya waandishi kuwa wahalifu kutokana na wanachokiandika kuhusiana na hali iliyoko, ni jambo linalokiuka uhuru wa kujieleza."
Waandishi wamekamatwa, wametukanwa na kupigwa
Michelle Bachelet, balozi wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya haki za binadamu kupitia kwa ujumbe alioutoa kwa njia ya video kwa washindi wa tuzo hiyo alisema "watu wanahitaji taarifa kamili na zisizo na makosa kuhusiana na janga hili na wanataka pia kuhusishwa katika maamuzi yanayofanywa kwa niaba yao. Na kwa muktadha huo, inashtusha kuona waandishi wakishambuliwa, wakitishiwa, wakikamatwa na hata kupotezwa kwasababu ya kuripoti kuhusu janga hili."
Mashirika ya waandishi wa habari yameripoti ukiukaji mkubwa wa uhuru wa waandishi wa habari katika janga hili la corona.
"Katika sehemu zote duniani, serikali za kidikteta zimetumia janga hili kuweka na kuongeza udhibiti wa vyombo vya kitaifa vya habari," Shirika la Waandishi wa Habari wasio na Mipaka lilisema katika taarifa.
Taasisi ya Kimataifa ya Uandishi wa Habari IPI ilirekodi zaidi ya visa 150 vya ukiukaji wa uhuru wa waandishi wa habari kote duniani katika mwezi mzima wa Aprili. IPI imefuatilia visa vya waandishi wa habari kunyimwa taarifa ila kulingana na taasisi hiyo ukiukaji mkubwa wa uhuru wa waandishi umekuwa katika kukamatwa, kutukanwa na kupigwa kwa waandishi hao.
Siogopi kufa
Hali ni ngumu zaidi hasa kwa waandishi walio katika nchi ambazo uhuru wa waandishi unadhibitiwa mno - kama vile China, nchi ambayo virusi viligundulika kwa mara ya kwanza mwezi Disemba 2019.
Shirika la Waandishi Wasio na Mipaka linasema, katika janga hili, dunia nzima imepata kuona athari za udhibiti kamili wa habari za China. Katika orodha ya mwaka huu ya Uhuru wa Uandishi wa Habari Duniani, China inashikilia nafasi ya nne kutoka mkiani.
Kupotea kwa waandishi kadhaa wa habari kutoka China waliokuwa wanaripoti kuhusu mripuko wa corona ni jambo lililogonga vichwa vya habari kote duniani. Kabla kupotea kwake Februari 6, wakili Chen Qiushi alitumia mtandao wa Twitter na Youtube kuwapa taarifa wafuasi wake kuhusiana na hali katika kituo cha karantini mjini Wuhan.
"Ninaogopa," Chen alisema katika vidio ambayo imeangaliwa zaidi ya mara milioni tatu kwenye mtandao wa Youtube, siku chache kabla kupotea kwake. "Ugonjwa wenyewe uko mbele yangu na polisi ya China na idara ya mahakama ziko nyuma yangu."
"Lakini mradi niko hai, nitaendelea kuripoti na kupeana kile nilichokiona na kukisikia mwenyewe," alisema. "Siogopi kufa. Chama cha Kikomyunisti, munafikiri ninawaogopa?"
Vitisho kutoka juu
Kisa cha Elena Milashina nchini Urusi pia kiliangaziwa kimataifa. Mwandishi huyo wa upekuzi aliyeshinda tuzo kadhaa amekuwa akiliandikia gazeti la Novaya gazeta tangu mwaka 1996. Milashina alianza kutafutwa na kiongozi wa kanda Ramzan Kadyrov kutokana na uandishi wake wa ukoasoaji kuhusiana na jinsi jamhuri ya Chechnya inavyoushughulikia mripuko wa virusi vya corona.
Katikati ya mwezi Aprili, Milashina aliandika taarifa kuhusiana na raia wa eneo hilo walio na dalili za ugonjwa wa Covid-19 kutokwenda hospitali kwa hofu ya kushambuliwa.
Na katika vidio iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii siku moja baadae, Kadyrov alivitaka vyombo vya usalama vya Urusi "kuwasitisha hawa watu wasio na utukuandika na kuwatusi watu wangu."
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yalitafsiri maneno hayo kama kitisho cha mauaji dhidi ya Milashina. Maneno ya Kadyrov pia yalisababisha serikali ya Ujerumani kupitia kamishna wa haki za binadamu Bärbel Kofler pamoja na balozi wa Ufaransa wa haki za binadamu Francois Croquette kuitaka Urusi kuchunguza vitisho hivyo dhidi ya Milashina.
DW inatoa wito wa kuachiwa kwa waandishi wote waliokamatwa
"Tunawakumbuka wenzetu wote ambao wanashurutishwa kutofanya kazi yao katika kipindi hiki kigumu," alisema Mkurugenzi Mkuu wa DW Peter Limbourg.
"Deutsche Welle inatoa wito wa kuachiwa mara moja kwa waandishi wote, kote duniani waliokamatwa kwasababu ya kuripoti kuhusu janga la Covid-19," aliongeza Limbourg.
Tangu mwaka 2015 Tuzo ya Uhuru wa Kujieleza ya DW imekuwa ikitolewa kila mwaka kwa juhudi au waandishi binafsi ambao wamechangia katika haki za binadamu au uhuru wa kujieleza.
Miongoni mwa walioishinda tuzo hiyo ni mwanablogu wa Saudi Arabia Raif Badawi, Chama cha Waandishi wa Ikulu ya WHite House pamoja na mwandishi wa habari wa Mexico Anabel Hernandez.
Kwa kawaida, sherehe ya kutolewa kwa tuzo hiyo ndiyo kilele cha Mkutano Mkuu wa Vyombo vya Habari Duniani unaofanyika kila mwaka mjini Bonn, ila kutokana na janga la corona, DW itaandaa mkutano huo mkuu kupitia vidio mwaka huu.