Uhusiano kati ya Pakistan na Marekani waathirika,kifo cha Osama
3 Mei 2011Vyombo vya habari nchini Pakistan vimesema leo kuwa kuuwawa kwa muasisi wa kundi la kigaidi la al-Qaeda Osama bin Laden katika shambulio lililofanywa na makomandoo wa jeshi la Marekani, kutaleta fadhaa kubwa kwa maafisa wa nchi hiyo .Maafisa wa Pakistan watakuwa katika mbinyo mkali kuelezea, vipi Osama alifanikiwa kuishi nchini humo bila kujulikana.
Baadhi ya wachambuzi wamedokeza kuwa Marekani itachukua hatua kuonyesha kutoridhishwa kwake na maafisa wa Pakistan.
Bin Laden alipigwa risasi mapema jana asubuhi na kikosi maalum cha jeshi la Marekani ambao waliingia kwa helikopta katika uwanja wa nyumba alimokuwa akiishi tangu mwaka 2005. Kwa muda mrefu amekuwa akifikiriwa kuwa amejificha katika ukanda wa eneo la makabila nchini Pakistan kaskazini magharibi karibu na mpaka na Afghanistan.
Rais Asif Ali Zardari, ameandika jana katika gazeti la Washington Post la Marekani , kuwa majeshi yake ya usalama hayakushirikishwa katika operesheni iliyofanyika usiku wa kuamkia Jumatatu. Lakini uwepo wa Bin Laden kilometa chache kutoka katika kituo kikuu cha jeshi , kunaweza kuharibu hadhi ya jeshi la Pakistan pamoja na upelelezi.
Kushindwa kwa Pakistan kugundua uwepo wa mtu huyo anayetafutwa sana duniani ni kitu kinachoshangaza, gazeti la News limesema katika uhariri wake.
Gazeti la Daily Times limeeleza nalo kuwa , vipi aliweza kujificha bila sisi kufanya kitu chochote , itakuwa vigumu kulieleza hilo kwa Wamarekani.
Gazeti la Dawn limesema kuwa operesheni ya kikosi cha jeshi la Marekani inaleta maswali kadha juu ya kiwango cha ushirikiano kati ya Marekani na jeshi pamoja na kitengo cha upelelezi nchini Pakistan.
Mshauri mkuu wa rais Barack Obama katika masuala ya ugaidi John Brennan amesema kuwa bado wanazungumza na maafisa wa Pakistan kuhusu uwepo wa Osama nchini humo.
Nadhani si kitu kinachoeleweka kwamba Osama hakuwa na mfumo wa usaidizi nchini humo, ambao ulimruhusu kukaa katika eneo hilo kwa muda mrefu. Sitaki kufikiria , ni aina gani ya msaada amepata kutoka kwa maafisa wa nchi hiyo. Na tunaacha nafasi wazi ili kuweza kuendelea kupata ushahidi zaidi.
Rais wa Pakistan Asif Ali Zardari amekana wasi wasi kuwa majeshi ya usalama ya nchi yake huenda yalikuwa yakisaidia kumficha Osama bin Laden. Asif Ali Zardari amesema kuwa majeshi ya Pakistan hayakushiriki katika operesheni siku ya Jumatatu dhidi ya Bin Laden lakini ushirikiano kati ya Pakistan na Marekani kwa muda mrefu umesaidia kuuwawa kwake.
Wakati huo huo Marekani imetangaza kuwa inasitisha huduma kwa jamii katika ubalozi wake pamoja na balozi ndogo nchini Pakistan, kutokana na wasi wasi wa kiusalama kufuatia kuuwawa kwa Osama bin Laden. Ubalozi wa Marekani mjini Islamabad pamoja na balozi ndogo katika miji wa Peshawar, Lahore na Karachi zimefungwa kwa shughuli za kawaida kwa umma kama vile utoaji wa visa na kadhalika hadi itakapotangazwa tena, amesema msemaji wa ubalozi Alberto Rodriguez.
Mwandishi : Sekione Kitojo / ape/afpe/ rtre
Mhariri :Mohammed Abdul-Rahman