1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhusiano wa Kongo na Rwanda waghubika siasa za Kongo

Idhaa ya Kiswahili9 Juni 2023

Mzozo wa Kongo na Rwanda umeghubika siasa nchini Kongo kabla ya uchaguzi wa rais, huku kukiwa na matukio ya kukamatwa kwa watu mashuhuri wa nchini humo wanaoshukiwa kushirikiana na maafisa wa Rwanda.

https://p.dw.com/p/4SOOr
Kuzuka upya kwa uasi wa kundi la M23 kulisababisha kuvunjika kwa ushirikiano baina ya Kongo na Rwanda
Kuzuka upya kwa uasi wa kundi la M23 kulisababisha kuvunjika kwa ushirikiano baina ya Kongo na Rwanda

Wakati tuhuma za kushirikiana na Rwanda zimekuwa kipengee muhimu cha siasa za Kongo kwa muda mrefu, hali ya wasiwasi imeongezeka katika wiki za hivi karibuni, kabla ya uchaguzi wa rais unaopangwa kufanyika tarehe 20 Desemba.

Wiki iliyopita wanajeshi walimkamata Salomon Kalonda, msaidizi wa mmoja wa wanasiasa wakuu wa upinzani nchini Kongo Moise Katumbi. Idara ya upelelezi ya kijeshi ilitangaza kuwa kukatwa kwa mwanasiasa huyo kunafuatia mawasiliano yake na waasi wa M23 na maafisa wa jeshi la Rwanda ili kuipindua serikali ya rais Tshisekedi.

Moise Katumbi, mfanyabiashara bilionea na gavana wa zamani wa jimbo la Katanga, anagombea katika uchaguzi wa urais. Chama cha Katumbi cha "Ensemble pour la Republique" kimekataa katakata shutuma dhidi ya Kalonda na kusema ni njama ya serikali kutaka kumzuia Katumbi kuwania urais.

Je, Tshisekedi anatumia Rwanda kama kisingizio cha kukandamiza upinzani ?

Wanasiasa wakuu wa Kongo Felix Tshisekedi, Moise Katumbu ( hapo juu) na Dr Denis Mukwege na Martin Fayulu
Wanasiasa wakuu wa Kongo Felix Tshisekedi, Moise Katumbu ( hapo juu) na Dr Denis Mukwege na Martin FayuluPicha: AFP/Getty Images, picture alliance, G. Kusema, DW

Kukamatwa kwa Kalonda kuna mwangwi wa kesi nyingine za hivi majuzi, ambazo zimeshuhudia kukamatwa kwa washauri wa rais Tshisekedi na majenerali wa jeshi kwa kile kinachoelezewa kuwa ni uhusiano wao na Rwanda.

Wafuasi wa rais Tshisekedi wamekuwa wakimtuhumu mpinzani Moise Katumbi kutoishutumu Rwanda katika kuwaunga mkono waasi wa M23. Waziri wa habari na msemaji wa serikali, Patrick Muyaya amesema wanasubiri kumuona Moise Katumbi akilaani kile alichoelezea kuwa ni uvamizi wa Rwanda nchini Kongo.

''Ukweli ni kwamba, hadi leo hatujamsikia Moise Katumbi akizungumza wazi kama Wakongo wengine dhidi ya uvamizi wa Rwanda, au dhidi ya rais Kagame. Ni muhimu aweke wazi msimamo wake, atuambiae ni upi msimamo wake kuhusu uvamizi wa Rwanda.'',alisema Muyaya.

Mnamo Januari, mshauri wa zamani wa Rais Felix Tshisekedi, Fortunat Biselele, alikamatwa kwa madai ya uhaini na tuhuma za uhusiano na Rwanda. Na mwezi Machi, mbunge wa Kongo Edouard Mwangachuchu, ambaye anawakilisha eneo la Masisi la Kivu Kaskazini alikamatwa kwa madai ya kuwa na uhusiano na waasi wa M23. Mmiliki huyo wa kampuni maarufu ya uchimbaji madini, Mwangachuchu kwa sasa anakabiliwa na kesi mjini Kinshasa.

Miongo miwili ya mahusiano ya panda shuka

Luteni Jenerali Philemon Yav, ambaye aliongoza operesheni ya kijeshi ya Kongo dhidi ya waasi wa M23 huko Kivu Kaskazini, alikamatwa Julai iliopita kwa tuhuma za uhaini mkubwa, na amekuwa akishikiliwa gerezani tangu wakati huo. Naye Francois Beya, mshauri maalum wa zamani wa Rais Tshisekedi anayehusika na usalama, alikamatwa Februari mwaka jana. Alishtakiwa kwa kula njama klwa kushirikiana na nchi jirani.

Toka utawala wa Joseph Kabila, suala la ushirikano wa Kongo na Rwanda limekuwa likighubika mijadala ya kisiaa nchini Kongo, hasa kupitia mitandao ya kijamii.