1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump autetea uhusiano kati ya Marekani na Saudia

21 Novemba 2018

Rais wa Marekani, Donald Trump amesema madai ya Saudi Arabia kuhusishwa katika mauaji ya mwandishi habari wa Saudia, Jamal Khashoggi, hayatoathiri uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

https://p.dw.com/p/38dIL
USA Washington Saudischer Kronprinz Mohammed bin Salman bei Donald Trump
Picha: picture-alliance/dpa/SPA

Akizungumza na waandishi habari jana, Trump amesema ingawa kamwe hawawezi kujua ukweli kamili wa mauaji ya Khashoggi, Marekani itaendelea kuwa mshirika imara wa Saudi Arabia.

Trump amekuwa katika shinikizo la kuiwekea vikwazo Saudia pamoja na mrithi wa kiti cha ufalme, Mohammed Bin Salman, ambaye ripoti ya Shirika la Ujasusi la Marekani, CIA ilieleza kuwa aliamuru mauaji ya Khashoggi. Trump amesema uchunguzi wa CIA haujakamilika kwa asilimia 100.

Amesema taifa hilo la kifalme ni mshirika muhimu na bado hajashawishika kama Bin Salman alihusika moja kwa moja na mauaji ya Khashoggi na huenda alijua kuhusu mauaji hayo au la, lakini amekataa kuitikia wito uliotolewa na wabunge wengi wakiwemo wa chama chake mwenyewe, kumtaka achukue hatua kali dhidi ya Saudia, ingawa amesema Marekani inalaani vikali mauaji ya mwandishi huyo wa habari.

Journalist Jamal Khashoggi
Mwandishi habari aliyeuawa, Jamal Khashoggi Picha: picture-alliance/AA/O. Shagaleh

Aidha, amesisitiza kwamba Marekani haitosimamisha mauzo ya silaha kwa Saudia, yenye thamani ya Dola bilioni 110. Rais huyo wa Marekani amesema kuifuta mikataba ya sihala kutazinufaisha nchini nyingine kama vile Urusi na China, hivyo asingependa kuuharibu uchumi wa nchi yake kutokana na uhusiano mbaya na Saudia, huku akiitetea sera yake ya ''Marekani Kwanza''.

Ujerumani kwa upande wake imesitisha mikataba ya silaha na Saudi Arabia na imewapiga marufuku raia 18 wa Saudia ambao wanaaminika kuhusika na mauaji ya Khashoggi kuingia nchini humo. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo ameuunga mkono uamuzi huo wa Trump, akisisitiza umuhimu wa uhusiano uliopo kati ya Marekani na Saudia.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu amesema bado wana maswali mengi na nchi yake itauomba Umoja wa Mataifa kufanya uchunguzi rasmi kuhusu mauaji ya Khashoggi.

Türkei Mevlut Cavusoglu, Außenminister in Ankara
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Mevlut CavusogluPicha: Getty Images/AFP/A. Altan

''Maswali yetu bado hayajajibiwa. Nani anahusika? Nani alitoa amri? Tunaamini kwamba watu hawa hawakuja tu Uturuki wenyewe kufanya mauaji. Lazima ijulikane wazi walitumwa na nani kufanya hivyo,'' alisema Cavusoglu.

Trump amekosolewa na vyombo mbalimbali vya habari pamoja na wanasiasa. Gazeti la Washington Post limesema Trump amekiuka maadili ya muda mrefu ya Marekani ya kuheshimu haki za binaadamu. Wabunge walioukosoa uamuzi wa Trump ni pamoja na Lindsey Graham, Rand Paul na Diane Feinstein.

Katika hatua ya kushangaza Trump aliipongeza Saudi Arabia kama mshirika imara katika kukabiliana na Iran dhidi ya mpango wake wa nyuklia pamoja na operesheni zake katika Mashariki ya Kati. Kauli hiyo imekosolewa vikali na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Javad Zarif ambaye ameshangazwa na hatua ya Trump kuitaja Iran wakati akijitetea kuhusu uovu uliofanywa na Saudia.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AP, AFP, Reuters
Mhariri: Bruce Amani