1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza, EU wapata rasimu ya muafaka wa Brexit

Daniel Gakuba
14 Novemba 2018

Muafaka umepatikana katika mazungumzo juu ya masharti ya Uingereza kuondoka katika Umoja wa Ulaya, na Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May anaanza kuwashawishi wabunge na mawaziri wake kuunga mkono makubaliano hayo.

https://p.dw.com/p/38CmO
Europa UK  l  Symbolbild Brexit
Picha: picture-alliance/dpa/Xinhua

Ofisi ya Waziri Mkuu May ilitangaza hapo jana kwamba wafanyakazi wa pande hizo mbili, Uingereza na Umoja wa Ulaya tayari wamekamilisha waraka wa muafaka huo.

Theresa May alikutana na mawaziri wake mmoja baada ya mwingine jana, na anatarajiwa kuitisha kikao cha baraza zima baadaye leo kuzungumzia muafaka uliofikiwa. Kulingana na msemaji wa serikali mjini London, amesema baraza la mawaziri ndilo litakaloamua hatua inayofuata.

Ikiwa baraza litaukataa muafaka huo uliofikiwa, Uingereza na Umoja wa Ulaya zitakuwa hazina makubaliano yoyote, huku tarehe ya mwisho ya Uingereza kuondoka rasmi katika Umoja wa Ulaya, tarehe 29 Machi 2019 ikikaribia.

Kizingiti katika baraza la mawaziri na bungeni

Kwa upande mwingine, ikiwa mawaziri watayaafiki makubaliano hayo, Uingereza itakuwa na nafasi nzuri ya kuitisha mkutano maalum wa Umoja wa Ulaya kuhusu Brexit, katika hatua za mwisho mwisho za kutalikiana na umoja huo.

UK Theresa May
Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May Picha: Getty Images/C. McQuillan

Kwa mujibu wa kituo cha utangazaji cha Jamhuri ya Ireland, makubaliano yamepatikana kuhusu mpaka baina ya Jamhuri hiyo na Ireland ya Kaskazini ambayo ni sehemu ya Uingereza. Mpaka huo umekuwa suala tete katika mazungumzo kuhusu Brexit.

Waziri Mkuu Theresa May amekuwa akikabiliwa na shinikizo kutoka nani ya chama chake na katika baraza lake la mawaziri kuhusu suala hilo la mpaka wa Ireland.

Kizingiti kikubwa kinamsubiri Bi May katika bunge, ambako wajumbe wengi wametishia kuukataa muafaka huo ikiwa hautazingatia masuala yenye kipaumbele kwao.

Corbyn na Johnson 

Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Leba, Jeremy Corbyn amesema atasubiri kujua kikamilifu yaliyomo katika makubaliano yaliyofikiwa, lakini akaongeza kwamba ana mashaka ikiwa yatakuwa mema kwa nchi.

Mpinzani mkubwa wa Theresa May kuhusu mwelekeo wa Brexit, waziri wa zamani wa mambo ya nchi za nje, Boris Johnson ambaye anatoka chama cha Theresa May cha Conservative, ametishia pia kuyapinga makubaliano hayo, akimshauri Theresa May kuachana nao.

Katika kura ya maoni ya Juni 2016, asilimia 52 ya wapiga kura nchini Uingereza waliunga mkono Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe, dpae

Mhariri: Caro Robi