1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza kuanza mazungumzo ya kuondoka EU

Jane Nyingi23 Septemba 2016

Uingereza inatarajia kuanza utaratibu wa kuupa talaka umoja wa ulaya mapema mwaka ujao.Waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Boris Johnson amesema hawahitaji miaka miwili kujadili utaratibu huo

https://p.dw.com/p/1K76Q
Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Boris Johnson
Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Boris JohnsonPicha: picture-alliance/AA/C. Bressan

Uingereza iko chini ya shinikizo kutoka mataifa mengine wanachama wa umoja huo kuondoka haraka iwezekanavo.Mataifa wanachama wa umoja wa ulaya bado yanasubiri uingereza kuwasilisha ombi rasmi la kujiondoa umoja huo kwa kuanza mazungumzo,chini ya ibara ya 50 ya mkataba wa Lisbon. Baada ya kuanza mazungumzo hayo uingereza itahitaji kipindi cha miaka miwili ili kujitoa kabisa EU. Wasaidizi wa waziri mkuu Theresa May wanasema matumaini yake ni mchakato huo kuanza mapema, ili kuondoa hofu yeyote katika chama chake tawala cha Conservative na pia miongoni mwa mamilioni ya wapiga kura.

Waingereza waliounga mkono kura ya Brexit
Waingereza waliounga mkono kura ya BrexitPicha: picture-alliance/dpa/A. Delvin

Hata hivyo baadhi ya wabunge na viongozi serikalini wanasema serikali bado haijapata muda wa kutosha kuweka vigezo vya kushiriki majadiliano hayo,na kwa kuanza mchakato huo mapema uingereza huenda,ikakosa kufaidi kutokana na majadiliano hayo.Katika mahojiano na kituo kimoja cha televisheni nchini Marekani waziri wa mambo ya nje ya Uingereza Boris Johnson aliondoa wasiwasi huo na kusema tayari inazungumza na mataifa wanachama wa EU kuhusu uhusiano wao katika siku za baadae."Huenda tukafaidi kutokana na nafasi zitakazojitokeza. Kikubwa ni kuhusu biashara huru na marafiki zetu katika umoja wa ulaya.Tunafanya hivyo pia kwa maslahi yao. Si sio tu hununua magari mengi kutoka ujerumani kuliko nchi nyingine yeyote katika umoja huo bali pia tunanua mvinyo kutoka Italia kuliko mataifa mengine bara Ulaya. Lita millioni 300 za Prosecco kila mwaka," alisema Johnson.

Johnson, ambae ni meya wa zamani wa mji wa London alikuwa miongoni mwa walioendesha kampeini ya kuwashawishi waingereza kupiga kura ya kuondoka Umoja wa ulaya.Waziri huyo ametupilia mbali mapendekezo kuwa Uingereza italazimika kuendelea kuruhusu usafiri huru wa watu wanaotoka mataifa ya umoja huo ili kuruhusiwa kuendelea kushiriki soko huru ndani ya bara la ulaya. .

Taarifa nyingine ni kuwa waziri mkuu Theresa May amekutana na rais wa bunge la Umoja wa Ulaya Martin Schulz ambae amemwomba kuharakisha mchakato wa uingereza kuondoka katika umoja huo kwa kuanza mazungumzo, chini ya ibara ya 50 ya mkataba wa Lisbon.

Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May (kushoto) na rais wa bunge la Umoja wa Ulaya Martin Schulz (kulia)
Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May (kushoto) na rais wa bunge la Umoja wa Ulaya Martin Schulz (kulia)Picha: picture alliance/AA/British Prime Ministry

Mwandishi: Jane Nyingi/rtre/ap

Mhariri: Daniel Gakuba