1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza kufahamu jina la waziri mkuu mpya

5 Septemba 2022

Uingereza itafahamu leo nani atayekuwa waziri mkuu, huku Liz Truss akipigiwa upatu kumrithi Boris Johnson na kuchukua usukani wakati nchi hiyo ikipambana na mzozo wa kuongezeka kwa gharama ya maisha

https://p.dw.com/p/4GPpp
BdTD | UK Belfast | Graffiti mit Kandidaten für den nächsten Premierminister | Rishi Sunak und Liz Truss
Picha: Paul Faith/AFP

Waziri wa mambo ya kigeni Truss na mpinzani wake, waziri wa zamani wa fedha Rishi Sunak, walitumia kipindi kizima cha msimu wa kiangazi kutafuta uungwaji mkono miongoni mwa wanachama wa chama cha Conservative ambao walipiga kura ya mwisho.

Soma pia: Mpambano wa kuwania uongozi Uingereza waanza rasmi

Kama atashinda, Truss atakuwa waziri mkuu wa Uingereza wa tatu mwanamke baada ya Theresa May na Margaret Thatcher. Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 47 amekuwa akiongoza dhidi ya Sunak mwenye umri wa miaka 42, katika uchunguzi wa maoni miongoni mwa wanachama karibu 200,000 wa Conservative wenye sifa ya kupiga kura.

Gazeti la The Sunday Times liliandika, yeyote atakayeibuka mshindi anakabiliwa na kibarua kikali muno cha kufanya kama waziri mkuu tangu enzi ya Thatcher.

Großbritannnien Liz Truss
Truss anapigiwa upatu kumpiku SunakPicha: Peter Nicholls/REUTERS

Uingereza inakabiliwa na mzozo mbaya zaidi wa gharama ya Maisha kuwahi kushuhudiwa katika vizazi vingi, huku mfumko ukipanda nazo bei za nishati zikiongezeka kutokana na vita vya Urusi nchini Ukraine

Soma pia: Nani atakua mrithi wa Johnson Uingereza?

Mamilioni wanasema kuwa huku gharama zikitarajiwa kupanda kwa asilimia 80 kuanzia Oktoba – na hata juu zaidi kuanzia Januari – wanakabiliwa na chaguo chungu kati ya kulan a kupasha joto majumbani wakati wa msimu wa baridi, kwa mujibu wa tafiti za maoni.

Aliliambia shirika la utangazaji la Uingereza BBC jana kuwa kama atachaguliwa kuwa waziri mkuu, atachukua hatua maramoja kuhusu gharama na usambazaji wa nishati. "Tunahitaji kushughulikia tatizo lilipo sasa, tunahitaji kuwasaidia watu, tunahitaji kuzisaidia biashara, lakini pia tunahitaji kuyatatua masuala ya usambazaji ambayo yametufanya kufika hapa tulipo sasa"

Truss amefanya kampeni kwa ahadi ya kupunguza kodi na kuweka kipaumbele kwenye ukuaji uchumi.

Sunak: Kudhibiti mfumko ni kipaumbele

London Politiker Rishi Sunak
Sunak alijiuzulu kama waziri wa fedhaPicha: Peter Summers/Getty Images

Sunak kwa upande wake aliapa kutoa msaada zaidi wa serikali kuwasaidia watu kulipia gharama zao za nishati na kusema kudhibiti mfumko litakuwa suala lake la kipaumbele, huku akiishambulia mipango ya Truss ya kupunguza kodi. "Kuna makundi matatu ya watu ambayo nimeyagawa. La kwanza ni kila mtu, kwa sababu nadhani kila mtu anahitaji msaada, ikizingatiwa ukubwa wa changamoto, na kisha makundi mengine mawili ya watu ambao watahitaji msaada zaidi, yani wale ambao wana kipato cha chini kabisa, karibu thuluthi ya kaya zote nchini, na kisha kundi la tatu la wastaafu."

Tangazo la leo litakalofanywa na maafisa wa Conservative la nani atachukua usukani uongozi wa chama litaanzisha mchakato wa matukio kadhaa.

Kesho Jumanne, Johson atatoa hotuba ya kuaga katika ofisi za waziri mkuu kwenye Mtaa wa Downing. Kisha atawasilisha rasmi barua yake ya kujiuzulu kwa Malkia Elizabeth II, ambaye naye atamteuwa mrithi wake katika hafla inayofahamika kama sherehe ya kubusu mikono.

Kwa mara ya kwanza katika utawala wake, Malkia huyo mwenye umri wa miaka 96 atamteuwa waziri mkuu katika kasri lake la mapumziko la Balmoral nchini Scotland, badala ya Kasri la Buckingham mjini London. Waziri Mkuu ajaye atakuwa wa 15 tangu Malkia huyo alipochukua kiti cha enzi.

afp