1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza: Kura muhimu kupigwa kuamua mchakato wa Brexit

6 Januari 2019

Bunge la Uingereza litapiga kura muhimu itakayoamua kuunga mkono au kuupinga mpango wa waziri mkuu Theresa May kuhusu mchakato wa Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/3B6AS
UK Theresa May Andrew Marr BBC
Picha: picture-alliance/ZUMA Press/V. Flores

Theresa May ameahidi kufanya bidii kubwa zaidi ili Uingereza ipewe mahakikisho zaidi kutoka Umoja wa Ulaya. Hata hivyo amesema mpango wa Brexit uliopo sasa ndio turufu ya mwisho.

Waziri Mkuu May alijaribu kuunadi mpango wake alipokuwa anazungumza katika mahojiano na shirika la televisheni la BBC leo, yaani takriban wiki moja kabla ya wabunge wa Uingereza kupiga kura muhimu ya kuamua juu ya mpango huo wa Brexit uliofikiwa baada ya mazungumzo baina ya waziri mkuu huyo na Umoja wa Ulaya la sivyo Uingereza italazimika kujiondoa Umoja wa Ulaya bila ya mkataba itakapofika tarehe 29 mwezi Machi.

Katika mahojiano hayo Theresa May alihakikisha kwamba mjadala juu ya kura muhimu bungeni, utaanza kufanyika wiki ijayo  kati tarehe 14 na 15. Bibi May aliahirisha kura hiyo ya wabunge mwezi uliopita baada ya  kubainisha kwamba mpango wake wa Brexit haukuwa unaungwa mkono na wabunge wa kutosha kutoka kwenye chama chake cha kihafidhina.

Wakati huo huo vyombo vya habari nchini Uingereza vinaamini kwamba wapambe wa waziri mkuu May wanaandaa mkakati ili mpango wa bibi May upitishwe bungeni lakini kwa masharti kwamba Umoja wa Ulaya unayaridhia zaidi matashi ya Uingereza.

Waziri Mkuu May ametahadharisha kwamba Uingereza itatumbukia mahala pasipokuwa na njia ikiwa, wabunge wataupinga mpango wake wa Brexit. Amesema hatari inayoweza kutokea ni Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya bila ya makubaliano.

Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May katikati akiwa na wajumbe wengine bungeni
Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May katikati akiwa na wajumbe wengine bungeniPicha: picture-alliance/House of Commons

Wakati huohuo amepinga miito juu ya kuitishwa kura nyingine ya maoni na amewataka wale wanaoyapinga makubaliano aliyofikia na Umoja wa Ulaya wawasilishe mpango mbadala. Ametilia maanani kwamba hadi sasa hakuna yeyote aliependekeza njia mbadala. Kulingana na mpango wa bibi May, mpaka wa Ireland kaskazini utaendelea kuwa wazi kwa muda, jambo linalopingwa vikali na mahasimu wanaoukataa mpango  wa Brexit wa waziri mkuu huyo.

Katika mahojiano hayo kiongozi huyo wa Uingereza alifafanua mambo matatu muhimu yatakayofanyiwa kazi mnamo wiki zijazo kwanza ni mpaka wa Ireland, pili, dhima kubwa zaidi ya bunge katika mazungumzo yatakayofanyika mnamo siku za usoni na tatu ni swala la kupata mahakikisho zaidi kutoka Umoja wa Ulaya juu ya uhusiano baada ya Uingereza kuondoka Umoja wa Ulaya. 

Hata hivyo  kiongozi huyo wa Uingereza amesisitiza  kuwa mpango  wa Brexit uliopo sasa mbele ya  wabunge ndiyo turufu ya mwisho. Theresa May amewaambia Waingereza kwamba Umoja wa Ulaya umeeleza wazi kuwa mpango wa Brexit uliofikiwa baina jumuiya hiyo na waziri mkuu wa Uingereza ndiyo  uliokuwapo mezani. 

Bibi May amesema mambo muhimu kwa wabunge kuyatilia maanani ni kuona iwapo mpango wa Brexit aliofikia na Umoja wa Ulaya unatimiza malengo ya kura ya maoni na iwapo unalinda maslahi ya wafanyabiashara na ya wananchi kwa jumla katika siku za usoni.

Mwandishi:Zainab Aziz/p.dw.com/p/3B5TI

Mhariri: John Juma