Uingereza: May aungwa mkono na mawaziri kuhusu Brexit
15 Novemba 2018
Ilichukua mazungumzo ya zaidi ya masaa matano, ambayo Bi May ameyaelezea kuwa ''marefu, yaliyogusa undani wa mambo, na yenye mjadala wa wazi.''
Katika taarifa fupi aliyoisoma kwa vyombo vya habari baada ya kukubaliana na mawaziri wake, Bi May alisema ana imani thabiti kwamba rasimu ya makubaliano ya kuondoka katika Umoja wa Ulaya ndio muafaka bora kabisa ambao ungeweza kufikiwa baina ya Uingereza na Umoja wa Ulaya.
Kizingiti kikubwa katika majadiliano juu ya mchakato wa Uingereza kupeana talaka na Umoja wa Ulaya, maarufu kama Brexit, kilikuwa juu ya mpaka kati ya Jamhuri ya Ireland ambayo inaendelea kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya, na Ireland ya Kaskazini, sehemu ndogo iliyo Kaskazini mwa kisiwa cha Ireland, ambayo ni himaya ya Uingereza.
Upo wasiwasi kwamba kurejeshwa kwa mpaka baina ya sehemu hizo, kunaweza kurudisha hisia za utaifa zinazoambatana na ghasia.
Kilichomo katika rasimu hiyo
Rasimu hii ya makubaliano kuhusu Brexit inaruhusu kipindi cha mpito cha miezi 21 kitakachoanza baada ya Uingereza kuondoka rasmi katika Umoja wa Ulaya, na kipengele cha kuibakisha Uingereza nzima katika muungano wa forodha wa Umoja wa Ulaya hadi pale mpango wa kudumu wa biashara baina ya pande hizo utakapopatikana.
Waziri Mkuu Theresa May alisema anaamini, kwa akili na moyo wake, kwamba uamuzi ulio katika rasimu hiyo ya makubaliano, unatilia maanani maslahi ya taifa la Uingereza.
Kufuatia maendeleo hayo nchini Uingereza, Rais wa Kamisheni ya Ulaya Jean Claude Juncker aliziandikia barua nchi 27 zinazobaki ndani ya Umoja wa Ulaya akiziomba kuunga mkono makubaliano ambayo aliyaita ''hatua muhimu.''
Kiongozi wa mazungumzo ya Brexit wa upande wa Umoja wa Ulaya Michel Barnier alisema makubaliano yaliyopatikana kuhusu mpaka wa Ireland ni tofauti na wazo lake la awali, lililonuia kuichukulia Ireland Kaskazini tofauti na sehemu nyingine za Uingereza, ambalo lakini lilikataliwa katakata na serikali ya London.
Upinzani wa ndani
Pamoja na yote hayo yaliyofikiwa, bado Theresa May anakabiliwa na kibarua kigumu kuweza kuileta pamoja nchi yake kukubali makubaliano hayo na Umoja wa Ulaya.
Chama cha Democratic Union, DUP cha Ireland ya Kaskazini chenye wabunge 10 wanaomuunga mkono Theresa May, kimesema makubaliano yaliyofikiwa hayaridhishi, na kwamba ni yale yale ambayo hapo awali Theresa May mwenyewe alisema asingeyakubali. Waziri Kiongozi wa Scotland, sehemu nyingine yenye mamlaka ya ndani nchini Uingereza Nicola Sturgeon, alizungumza kwa simu na Waziri Mkuu Theresa May, na kulalamika kwamba makubaliano hayo hayatilii maanani maslahi ya Scotland.
Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Leba Jeremy Corbyn pia ameiponda rasimu hiyo ya makubaliano kuhusu Brexit, akisema sio yenye tija kwa sababu hayazingatii mahitaji ya maeneo yote ya nchi. Hata hivyo, upinzani mkali zaidi unaomkabili Theresa May, unatoka ndani ya chama chake cha Conservative.
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas amekaribisha hatua iliyofikiwa, na kuongeza kwamba Ujerumani inasikitishwa na kuondoka kwa Uingereza ndani ya Umoja wa Ulaya.
Mwandishi: Daniel Gakuba/dpae,rtre
Mhariri:Caro Robi