Uingereza: May na baraza lake waafikiana kuhusu Brexit
7 Julai 2018Makubaliano hayo yalifikiwa katika mkutano wa saa kadhaa uliofanyika katika makazi ya waziri mkuu ya Chequers yaliyo nje ya mji mkuu, London jana Ijumaa. Bi Theresa May alikuwa akijaribu kuwianisha mtazamo wa mawaziri wake kuhusu uhusiano wa kiuchumi baina ya Uingereza na Umoja wa Ulaya, baada ya mchakato wa Brexit kukamilika. Kulikuwa na mgawanyiko mkubwa katika baraza hilo.
''Huu ni mpango ambao naamini utakuwa mzuri kwa Uingereza na pia kwa Umoja wa Ulaya na natarajia kwamba utaungwa mkono.'' Bi May aliwaambia waandishi wa habari Ijumaa jioni.
Ushindi wa kila upande
Kulingana na mpango huo ulioafikiwa, Uingereza itajiondoa katika sekta nyingi za soko la pamoja katika Umoja wa Ulaya, na umoja wa forodha kwa bidhaa na huduma. Unanuia pia kuiondoa nchi hiyo chini ya sheria ya Umoja wa Ulaya, ili kuiruhusu kuingia mikataba binafsi na nchi nyingine nje ya Umoja wa Ulaya. Azimio jingine muhimu ni kuondoa uhuru wa watu kusafiri kutoka Umoja wa Ulaya kuingia Uingereza.
Wale wenye misimamo mikali kuhusu Brexit katika chama cha Conservative cha Theresa May walikuwa wakipigia debe mpango wa Uingereza wa kujitenga kabisa, ili ishughulikie kwa uhuru kamili masuala yanayohusu biashara na uhamiaji.
Mpango uliofikiwa lakini unaonekana pia kuzingatia matakwa ya wale wanaotaka mafungamano zaidi na Ulaya ndani ya chama cha conservative. Aidha, unazitaka pande zote hizo mbili kupata muafaka mpya kuhusu namna Uingereza itakavyohusiana na soko huria la Umoja wa Ulaya na muungano wake wa forodha. Hili linatilia maanani Uingereza kuendelea kuzitengeneza bidhaa zake kukidhi viwango vya Umoja wa Ulaya.
Kuhusu mpaka na Umoja wa Ulaya kati ya Jamhuri ya Ireland na Ireland ya Kaskazini
Bidhaa zinazopitia Uingereza lakini zikiwa njiani kuingia katika nchi mwanachama wa Umoja wa Ulaya hazitawekewa vizuizi, hii ikiwa kulingana na makubaliano yaliyopatikana. Mahali bidhaa zinakoelekea patajulikana kwa kutumia teknolojia ya kutathmini masharti ya biashara na ushuru, ambayo itapatikana mpakani.
Waziri Mkuu Theresa May amesema anayo matumaini kwamba makubaliano haya yataridhisha matakwa ya Umoja wa Ulaya, ya kuepuka ukaguzi wa mpakani kati ya Ireland ya Kaskazini, ambayo ni sehemu ya Uingereza, na Jamhuri ya Ireland, ambayo ni mwanachama wa Umoja wa Ulaya.
Mpango uliopendekezwa hata hivyo, unatenga kando sekta ya huduma, ambayo ni mihumu sana kwa uchumi wa Uingereza, kuipa nchi hiyo uhuru mkubwa wa maamuzi mara tu itakapokamilisha mchakato wa kuondoka ndani ya Umoja wa Ulaya mwezi Machi mwaka ujao wa 2019.
Kupitia ukurasa wake wa twitter, afisa mkuu wa Ulaya katika mazungumzo ya Brexit Michel Barnier, amesema atayachunguza mapendekezo hayo ya Uingereza, kuangalia kama yanatekelezeka.
Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre, dpae
Mhariri:Sekione Kitojo