Uingereza na EU zaafikia rasimu ya makubaliano kuhusu Brexit
23 Novemba 2018Rais wa baraza la Umoja wa Ulaya Donald Tusk amesema rais wa halmashauri ya Umoja huo Jean Claude Juncker amemuarifu kuwa wajumbe wanaoshiriki katika mazungumzo hayo ya Brexit wamekubaliana kuhusu suala la kisiasa wakisubiri sasa makubaliano hayo kuidhinishwa na viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya wanaotarajiwa kukutana katika mkutano maalum wa kilele Jumapili hii.
Tusk amesema rasimu hiyo ya kurasa 26 imeshughulikia masuala ya kibiashara, usalama, mazingira, miongoni mwa masuala mengine na sasa itapelekwa kwa nchi nyingine 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya kuidhinisha.
Uingereza yapiga hatua kuelekea Brexit
Azimio la kisiasa lililofikiwa linasema mahusiano ya siku za usoni yatakuwa mapana yakihusisha ushirikiano wa kiuchumi, sheria, sera za kigeni, usalama na ulinzi.
Pia inajumuisha Uingereza kuanzisha sera huru ya kibiashara na kusitishwa kwa uhuru wa kuingia na kutoka kwa raia wa Umoja wa Ulaya nchini Uingereza - na raia wa Uingereza kuingia katika nchi za Umoja wa Ulaya, mambo mawili makuu ambayo yalisababisha nchi hiyo kupiga kura ya maoni ya kujiondoa kutoka Umoja wa Ulaya mwaka 2016.
Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May ameyataja makubaliano hayo kuwa mazuri zaidi kwa Uingereza na kusema mashauriano yamefikia hatua nyeti, huku akiendelea kukosolewa vikali na wanasiasa wa upinzani bungeni kuhusiana na kufikia rasimu ya makubaliano ambayo kwao yanaendeleza mahusiano ya karibu kati ya Uingereza na Umoja wa Ulaya baada ya Brexit.
Lakini makubaliano hayo yaliyofikiwa Alhamisi hayakuangazia suala tete la haki za uvuvi na eneo la Gibraltar ambayo yamezua tofauti hasa kati ya Uingereza na Uhispania.
Uhispania bado ina mashaka na Brexit
Baada ya makubaliano hayo kufikiwa, Waziri mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez ameonya tena kuwa nchi yake itayapinga makubaliano ya Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya ikitumia kura ya turufu, kwa sababu ya suala la Gibraltar, eneo linalosimamiwa na Uingereza na ambalo Uhispania kwa muda mrefu imekuwa ikidai ni ardhi yake.
Sanchez amesema baada ya kufanya mazungumzo na May hapo jana, misimamo yao haijabadilika na kusisitiza kama makubaliano hayo hayatafanyiwa mabadiliko kushughulikia hatma ya Gibraltar, basi atatumia kura ya turufu kupinga Brexit.
Mbali na Uhispania kutishia kutumia kura ya turufu, bunge la Uingereza pia linaweza kupinga makubaliano hayo yaliyopatikana. Waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Uingereza Boris Johnson amesema rasimu hiyo inapuuza kabisa lengo la Brexit.
Kiongozi wa chama cha upinzani cha Leba Jeremy Corbyn amethibitisha kuwa chama chake hakitaunga mkono makubaliano hayo akiyataja mabaya zaidi kuwahi kufikiwa duniani na kuyafananisha na kuruka gizani ukiwa umefungwa macho.
Naye waziri wa fedha wa Ujerumani Olaf Scholz amesema Ujerumani inatumai Uingereza itaondoka kwa njia ya mpangilio lakini imejiandaa iwapo nchi hiyo itaondoka bila ya ya makubaliano kufikiwa na pande zote.
Mwandishi: Caro Robi/Afp/Reuters/Ap
Mhariri: Gakuba, Daniel