1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Awamu ya tatu ya mazungumzo ya kibiashara ya Brexit yaanza

11 Mei 2020

Uingereza na Umoja wa Ulaya zinaanza awamu ya tatu ya mazungumzo ya kibiashara huku kukiwa na matumaini madogo ya kufikia mwafaka, wakati pande hizo zikikabiliwa na changamoto ya virusi vya corona .

https://p.dw.com/p/3c2NQ
Bildkombo David Frost, UK Brexit-Unterhändler & Michel Barnier, EU-Kommission

Mazungumzo hayo mapya yanafanyika  kwa njia ya video kati ya mjumbe mkuu wa Umoja wa Ulaya katika suala la Brexit Michel Barnier na mwenzake wa Uingereza David Frost, wote wawili wakiwa wamepona ugonjwa wa COVID-19.Mkutano huo utafuatiwa na misururu ya mikutano ya wiki nzima pia kwa njia ya video  itakayowahusisha mamia ya maafisa waandamizi.

Uingereza ilijiondoa katika Umoja wa Ulaya Januari 31 na pande zote mbili zina muda wa hadi mwishoni mwa mwaka huu kupata mpango mpya wa uhusiano kati yao na kuzuia kuongezwa kwa muda ambao waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson amekataa kuuzingatia.

Mazungumzo kwa njia ya video ya awamu za awali yalivunjika Aprili 24 bila ya kupatikana kwa ufanisi mkubwa. Mazungumzo hayo yalifuatia awamu ya kwanza na kufikia sasa ndio ya pekee ya ana kwa ana yalioandaliwa mnamo mwezi Machi.Upande wa Umoja wa Ulaya unailaumu uingereza kwa kuzingatia tu masuala yenye umuhimu kwao na kupuuza yale yalio na umuhimu kwa wanachama wa Umoja huo kama vile uvuvi ama makubaliano kuhusu viwango vya afya na mazingira. 

Großbritannien Boris Johnson
Waziri mkuu wa Uingereza- Boris JohnsonPicha: picture-alliance/dpa/S. Rousseau

Kamishna wa masuala ya kibiashara wa Umoja wa Ulaya Phil Hogan, alilalamika akisema hakuona dalili kuwa Uingereza inafanya mazungumzo ikiwa na azma ya kupata matokeo yenye tija. Uingereza kwa upande wake inasema imejitolea kikamilifu katika mazungumzo hayo. Msemaji mmoja wa nchi hiyo amesema hawayatambui madai ya kwamba wamekuwa hawajihusishi na mazungumzo na Ulaya kuhusu sekta yoyote, na kuongeza kuwa Uingereza itaendelea kujadiliana kutafuta suluhisho litakaloangazia uhalisia wa kisiasa wa pande zote mbili.

Shutma nyingine ni kwamba Uingereza inajivuta katika utekelezaji wa masuala muhimu ya kujiondoa kwake katika umoja huo. Hii inahusiana na kuweka vizuizi kati ya Ireland ya Kaskazini na maeneo mengine ya Uingereza, mpaka ulioko ukiwa ni bahari ya Ireland ambayo Uingereza iliikubali tu mwishoni mwa mazungumzo ya kujiondoa katika Umoja huo.

Kutokana na vikwazo vilivyowekwa na athari nyingine zilizoko kuhusiana na virusi vya corona, utabiri katika Umoja wa Ulaya ni kwamba ufanisi utapatikana tu karibu na muda wa mwisho uliowekwa  wakati Uingereza itakapotumia mzozo ulioibuka kuhalalisha mabadiliko ya ghafla kwa muda wa mwisho.

Iwapo hakuna mkataba utakaoafikiwa kufikia Desemba 31, basi sheria za shirika la biashara duniani zitaanza kutumika huku kukiwa na viwango vya juu vya kodi na vikwazo vya forodha kati ya Uingereza na Umoja wa Ulaya.