Uingereza yaziwekea vikwazo kampuni zenye ushirika na Urusi
8 Agosti 2023Uingereza imeidhinisha vikwazo dhidi ya kampuni ya Iran inayotengeneza ndege zisizo na rubani, pamoja na kampuni nyingine kadhaa za kigeni zinazopeleka silaha na nyenzo nyingine za kijeshi zinazotumika dhidi ya Ukraine. Uingereza, Marekani na Umoja wa Ulaya zimeshaweka vikwazo vya aina mbalimbali tangu mwezi Februari ili kuiadhibu Urusi kwa ajili ya uvamizi wake nchini Ukraine.
Serikali ya Uingereza imeweka vikwazo vipya 25 dhidi ya watu binafsi na makampuni ya nchini Iran, Uturuki, Belarus, Slovakia, Uswisi, Umoja wa Falme za Kiarabu na Urusi yenyewe. Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza James Cleverly amesema vikwazo vya leo ambavyo ni vya kihistoria vitapunguza zaidi, uwezo wa kisilaha wa Urusi na kuufunga mtandao wa ugavi unaompa nguvu Rais Putin, na sekta ya ulinzi ambayo sasa inatatizika. Vikwazo vilivyotangazwa leo vinapiga marufuku kampuni za Uingereza kufanya biashara na kampuni zilizowekewa vikwazo.