Sheria mpya za uhamiaji Uingereza itakapojitenga na EU
2 Oktoba 2018Uingereza kupitia Waziri wake Mkuu Theresa May imesema raia wote wa Mataifa ya Ulaya wanaweza kwa sasa kuishi na kufanya kazi nchini Uingereza lakini hilo litabadilika baada ya nchi hiyo kuondoka mwaka ujao katika muungano wa nchi 28 unaounda Umoja wa Ulaya.
May Amesema Uingereza itabakia nchi yenye wazi lakini kwa mara ya kwanza itakuwa na udhibiti wa kuchagua nani inayomtaka kuingia nchini humo.
Akizungumza leo siku ya Jumanne katika mkutano wa kila mwaka wa chama chake cha Conservatives ulioanza siku ya Jumapili, May amesema anajitayarisha kutoa pendekezo jipya kwa Umoja wa Ulaya linalonuiwa kuvunja kizingiti kilichopo katika majadiliano ya Brexit.
Huku hayo yakiarifiwa Waziri wa zamani wa mambo ya kigeni Boris Johnson leo vile vile anatarajiwa kupinga mpango wa Theresa May katika hotuba yake inayosubiriwa kwa hamu ambayo wengi wanaiona kama njia moja ya kutaka nafasi ya May.
Johnson alijiuzulu katika serikali ya May mwezi Julai kutokana na pendekezo la Waziri Mkuu huyo la kutaka mahusiano ya karibu zaidi ya kibiashara na Umoja wa Ulaya baada ya Brexit.
Tangu wakati huo amekuwa mpinzani mkali wa May huku akionekana kujipigia debe juu ya ujuzi wake wa kuongoza.
Hata hivyo Theresa May amedokeza kuwa yuko na ataendelea kuwepo katika nafasi yake hiyo kwa muda mrefu huku akikiomba chama chake cha conservatives kuungana na kumuunga mkono katika mapendekezo yake ya Brexit.
Waziri Mkuu huyo anakihitaji sana chama chake ili apate makubaliano ya mwisho bungeni kabla mwezi Machi mwaka Ujao siku ambayo Uingereza itauaga Umoja huo wa Ulaya.
Kwengineko kiongozi wa chama kidogo cha Ireland ya Kaskazini DUP Arlene Foster anaeiunga mkono serikali ya May amesema ataangalia mapendekezo yote mapya kwa Umoja wa Ulaya kuhusu mpaka wa Ireland.
Arlene Foster amesema Ireland ya Kaskazini itapaswa iondoke kwa masharti yale yale kama Uingereza.
Muandishi: Amina Abubakar/dpa/AFP/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman