Uingereza yaahidi kuihakikishia Ukraine usalama
16 Januari 2025Akiwa katika ziara yake ya kwanza nchini Ukraine tangu kuchukua wadhifa wa uwaziri mkuu Julai mwaka jana, Starmer alisisitiza msaada wa Uingereza kwa Ukraine na kutoa ahadi ya ushirikiano wa miaka 100 na Rais Volodymyr Zelenskiy.
Ziara hii, ambayo ilifanyika siku chache kabla ya Donald Trump kurudi madarakani Marekani, ilijikita katika kuhakikisha Ukraine inakuwa kwenye nafasi thabiti kupambana na Urusi mwaka 2025.
Katika mazungumzo yaliyokatizwa na mlipuko uliosababishwa na mifumo ya ulinzi wa anga wa Ukraine kudungua droni ya Urusi karibu na ikulu ya rais, Zelenskiy alizungumzia haja ya kupelekwa kwa vikosi vya kulinda amani vya Magharibi ili kuzuia mashambulizi ya siku za usoni ya Urusi baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano.
Starmer aliahidi kuwa Uingereza itatafakari njia za kivitendo za kufanikisha amani ya haki na endelevu ambayo italinda usalama, uhuru, na haki ya Ukraine kuchagua mustakabali wake.