Uingereza yakasirishwa Marekani kuvujisha taarifa
25 Mei 2017Hatua hiyo ni kwasababu ya hofu ya kuvuja kwa taarifa hizo katika vyombo vya habari nchini Marekani ambako kunaweza kuzuwia msako wa kumtafuta mtu ambaye huenda amehusika katika utengenezaji wa bomu ambaye hadi sasa hajapatikana.
Iwapo itathibitishwa , hatua hiyo ya kuzuwia kupeana taarifa na mshirika muhimu kabisa wa Uingereza katika ulinzi na usalama kutaonesha kiwango cha hasira ya Uingereza kuhusiana na kuvuja katika vyombo vya habari nchini Marekani kuhusu taarifa za uchunguzi wa polisi.
Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May atalizusha suala hilo wakati wa mkutano wake na rais wa Marekani Donald Trump leo, vyanzo katika serikali vimelieleza shirika la habari la Reuters, baada ya gazeti la New York Times kuchapisha picha za eneo lililotokea mashambulizi mjini Manchester ambako watu 22 waliuwawa.
Picha hizo ni pamoja na mabaki ya bomu linaloshukiwa kutumiwa katika shambulio hilo, mfuko wa kubeba mgongoni uliokuwa umebebwa na mshambuliaji wa kujitoa muhanga na kuonesha damu katika mabaki ya magari yaliyoharibiwa.
Kuvuja kwa taarifa
Shirika la utangazaji la BBC limesema polisi ya Manchester inamatumaini ya kurejesha uhusiano wa kupashana habari za kijasusi hivi karibuni lakini kwa sasa imekasirishwa.
Baada ya shambulio baya kabisa kuwahi kuwauwa watu nchini Uingereza tangu mwaka 2005, polisi imo katika msako kumtafuta mshirika ambae inashuku alimsaidia Salman Abedi kutengeneza bomu hilo lililowauwa watu 22 siku ya Jumatatu katika ukumbi wa tamasha la muziki uliojaa watu kaskazini mwa mji nchini Uingereza wa manchester.
Salman Abedi , mshambuliaji wa kujitoa muhanga raia wa Uingereza , alikuwa nchini Ujerumani siku nne kabla ya shambulio hilo siku ya Jumatatu, limeripoti shirika la habari la Sky , likinukuu taarifa za kijasusi za Ujerumani. Abedi alikuwa katika mji wa Dusseldorf , ambao uko kilometa 300 magharibi mwa mji mkuu Berlin.
Uhusiano na mshambuliaji
Wachunguzi wanaonesha kwamba Abedi alikuwa sehemu ya mtandao mpana wa wanamgambo. Kile kinachowapa hofu majirani wa Abedi hivi sasa ni uhusiano ambao haujulikani kati ya mshambuliaji na ndugu zake ambao ni washukiwa na kati ya shambulio hilo na imani yake. Wakati baba yake Abedi na ndugu zake wanashikiliwa kwa ajili ya uchunguzi , waandishi habari wamekwenda katika msikiti mkubwa mjini Manchester kutaka kujua ushahidi wa kuhusika katika shambulio hilo. Mfanyakazi mmoja wa msikiti huo amesema:
"Sifurahii kabisa kwa kweli, kwasababu kwa sehemu fulani wanahusisha tukio hili na Uislamu. Huu sio Uislamu, Haiwakilishi Uislamu. Sidhani wanapaswa kuwa hapa."
Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May atasimamia kikao cha kamati ya serikali inayochukua hatua za dharura leo , amesema msemaji wa ofisi yake. May ambae anatarajiwa kwenda mjini Brussels baadaye leo kwa ajili ya mkutano wa jumuiya ya NATO amekuwa na mikutano kadhaa ya kamati hiyo tangu shambulio hilo kufanyika siku ya Jumatatu.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Yusuf Saumu