Uingereza yaongeza kasi kuelekea wasi wasi kuhusu Brexit
21 Februari 2019Hadi pale waziri mkuu Theresa May atakapoweza kupata makubaliano ya Brexit yatakayoidhinishwa na bunge la Uingereza, hapo ndio atakapoweza kuamua iwapo kuchelewesha Brexit ama aliingize taifa hilo lenye uchumi wa tano mkubwa duniani katika mkanganyiko kwa kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya bila ya makubaliano hapo Machi 29.
Waziri mkuu Theresa May hata hivyo amesema amepiga hatua katika mazungumzo na Umoja wa Ulaya jana wakati akitafuta kupata madhiriano zaidi katika masharti ya Uingereza kujitoa, lakini kama ilivyotarajiwa hakukuwa na mafanikio makubwa.
"Nilikuwa na mkutano mzuri na rais Juncker jioni hii. Nilisisitiza haja ya kuona mabadiliko yenye uwezo wa mabadiliko ya kisheria katika suala la mpaka kuhakikisha kwamba hautakuwa wa milele. hicho ndio kinachohitajika iwapo makubaliano yatapita katika baraza la wawakilishi. Tumekubaliana kwamba kazi ya kutafuta suluhisho itafanyika haraka."
Alipoulizwa kitu gani kitatokea wiki ijayo, waziri wa fedha Philip Hammond alisema kwamba huenda kutakuwa na fursa ya kulipigia kura suala hilo bungeni, kunaweza kuwa na fursa, lakini hilo litaweza kutokea kwa kutegemea hatua za maendeleo ambazo zitafikiwa katika siku chache zijazo.
Hofu inaongezeka
May , ambaye mwanzo alikuwa akisita sita kuunga mkono uanachama wa Umoja wa Ulaya ambaye alifanikiwa kuchukua uongozi huo wa juu katika mtafaruku wa kisiasa kufuatia kura ya maoni mwaka 2016, aliahidi kuwapa wabunge fursa ya kuamua kile kinachotakiwa kufanyika juu ya Brexit hapo Februar 27, hadi pale atakapoweza kurejesha tena makubaliano hayo.
Hofu inaongezeka kwamba Uingereza inaweza kujitoa bila ya makubaliano, na kumekuwa na hali nyingine ya mtafaruku kabla ya may kwenda Brussels wakati wabunge wake watatu walipojiuzulu kutoka chama cha Conservative wakipinga kuhusu Brexit na kujiunga na kundi jipya huru la wabunge.
May amesema waziri wake wa Brexit Stephen Barclay na mwanasheria mkuu Geoffrey Cox watakwenda Brussels leo , siku tatu tu tangu walipofanya ziara ya mwisho, wakati kasi ya majadilino ikiongezeka.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre
Mhariri:Yusuf Saumu