Uingereza yaongoza kwa vifo vingi vya COVID-19 Ulaya
5 Mei 2020Uingereza inaonekana kuipiku sasa Italia kwenye nafasi ya taifa lililoathiriwa vibaya kabisa na COVID-19. Awali serikali ilikuwa imesema watu 28,734 wamekufa kwa ugonjwa huo wakiwa hospitalini, nyumba za wazee na maeneo mengine, huku Italia ikiripoti vifo 29,079.
Idadi hii, hata hivyo, inatajwa kuwa ni chini ya uhalisia, kwani inajumuisha wale tu waliopimwa na kukutwa na maambukizo hayo, ilhali vipimo havikuwa vimefanywa kwenye nyumba za kutunzia wazee kwenye mataifa yote mawili hadi hivi karibuni kabisa.
Bali kufikia mchana wa leo, Uingereza ilichapisha takwimu mpya ambazo zilitaja idadi ya waliokwishapoteza maisha saa imefikia 30,000. Na hii ni idadi ya hadi tarehe 24 Aprili, takribani wiki moja na nusu iliyopita.
Hali pia inazidi kuwa mbaya nchini Urusi, ambako idadi ya walioambukizwa imepanda kwa kasi, hasa katika mji mkuu, Moscow, ambao umeripoti zaidi ya wagonjwa 10,000 ndani ya siku tatu mfululizo.
Hilo, hata hivyo, halijazuwia nchi nyingi hapa Ulaya kulegeza masharti ya zuwio kwenye shughuli za kawaida.
Kuanzia Jumatatu (Mei 4), Italia iliwaruhusu watu milioni nne na laki nne kurejea kazini na kulegeza masharti ya kutembea kwa mara ya kwanza ndani ya kipindi cha miezi miwili.
Wimbi jipya la maambukizi laja
Wanasayansi wamewaonya wanasiaa wajitayarishe na wimbi jipya la maambukizi. Mkuu wa Taasisi ya Robert Koch ya hapa Ujerumani, Lothar Wieler, amesema kuwa wanasayansi wana wasiwasi kuwa kunaweza kuwapo hata wimbi la tatu la maambukizo, ambayo yatawakumba watu wengi zaidi.
Wiki chache kutoka sasa zinatazamwa na wanasayansi kama kipindi cha majaribio ya kupima ni kwa namna gani jitihada za kuzuwia maambukizo mapya zinashabihiana na hatua ya mataifa kadhaa ya Magharibi kufungua tena chumi zake, kwa mujibu wa mkuu wa taasisi ya maradhi ya maambukizo nchini Italia, Daktari Giovanni Rezza, ambaye ameliambia gazeti la La Repubblica kwamba asingelipenda kuona kuwa watu wanadhani kuwa janga limemalizika, kwani bado lingalipo.
Kwa upande wa China, hii inaingia wiki ya tatu bila ya taifa hilo la Asia, ambalo ndiko maradhi haya yalikoanzia, kuripoti kifo kinachotokana na virusi vya korona.
Kwa mujibu wa wizara ya afya, kuna mgonjwa mmoja tu mpya aliyethibitishwa kuambukizwa na huku wagonjwa wasiofikia 400 wakiwa wanatibiwa kwa sasa.
Maeneo mengine ya Asia na Pasifiki yanaripotiwa pia kuanza kuona mafanikio ya kushuka kwa maambukizo, zikiwemo Hong Kong, Taiwan, Vietnam, Thailand, Australia na New Zealand, ambayo kwa siku mbili mfululizo haijaripoti mgonjwa mpya.
Hata hivyo, India, taifa lenye wakaazi bilioni 1.3 limesema bado halijafikia kilele cha maambukizo hadi sasa.