Viongozi wa EU watafuta makubaliano juu ya madai yaUingereza
19 Februari 2016Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron ambaye anapata shinikizo kutoka makundi ya wasiopenda Umoja wa Ulaya katika chama chake cha Conservative, na pia kutoka vyombo vya habari vyenye mrengo wa kizalendo anasema anaweza kuunga mkono kura ya kutaka Uingereza iondoke ndani ya Umoja wa Ulaya katika kura ya maoni inayotarajiwa, iwapo hatapata mageuzi anayoyataka katika umoja huo.
Lakini kufuatia wasiwasi ilionao Ufaransa na mataifa mengine ya Mashariki mwa Ulaya, Rais wa Baraza la Ulaya Donald Tusk ameonya kuwa bado ipo njia ndefu ya mazungumzo kufikia makubaliano ya kuizuwiya Uingereza isijitoe ndani ya Umoja wa Ulaya.
"Kwa sasa naweza kusema kwamba tumepiga hatua kidogo, lakini bado kuna mengi yanayohitajika kufanywa," alisema Donald Tusk.
Kwa upande wake kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameonekana kuunga mkono msimamo wa waziri mkuu wa Uingereza David Cameroon wakati Ulaya ikijaribu kudumisha umoja wake, ili iweze kushughulikia tatizo jengine la mgogoro wa wakimbizi.
"Makubaliano sio rahisi kufikiwa lakini nia ipo, tuko tayari kuafikiana kwa sababu faida ni nyingi kuliko hasara wakati Uingereza ikibakia katika umoja wa Ulaya," amesema Merkel alipozungumza na waandishi habari.
Makubaliano huenda yakachukua muda mrefu kuliko inavyodhaniwa.
Lakini Waziri Mkuu wa Ireland Enda Kenny ameonya kuwa makubaliano yanaweza kuchukua muda mrefu kuliko inavyofikiriwa. Cameron, amesema iwapo mageuzi mwafaka hayatapatikana lolote linawezekana, huku akikana kukiri uwezekano wa Uingereza kuwa nchi ya kwanza kuondoka katika Umoja huo zaidi ya miaka 60 ya historia yake.
Waziri Mkuu huyo wa Uingereza ameongeza kuwa nchi yake haitaki kuvunja daraja na kujitenga na ulimwengu, na kuongeza lakini kuwa hali ya mashaka ndani ya Umoja wa Ulaya inazidi kuongezeka kila uchao.
Huku muda ukiyoyoma wa kufikia makubaliano katika siku ya mwisho ya mkutano wa Brussels Donal Tusk amefanya mazungumzo ya ana kwa ana na Cameron pamoja na Mkuu wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker usiku wa kuamkia leo ili kujaribu kuafikiana. Tusk pia alikutana na rais wa Ufaransa Francois Hollande, Waziri Mkuu wa Ubelgiji Charles Michel ana mwenzake wa Jamhuri ya Czech Bohuslav Sobotka.
Kwengineko Umoja wa Ulaya umepanga kuandaa mkutano maalum na Uturuki mapema mwezi Machi kuzungumzia mgogoro wa wakimbizi. Kwa mujibu wa rais wa baraza la Ulaya Donald Tusk mpango wa kuzuwiya mmiminiko wa wakimbizi katika mataifa ya ulaya unabakia kuwa muhimu na ni lazima wafanye kila wawezalo ili wafanikiwe.
Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/dpa
Mhariri: Gakuba Daniel