1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza yatakiwa ibadilishe mkakati katika suala la Brexit

Zainab Aziz Mhariri: Sekione Kitojo
13 Machi 2019

Licha ya mpango wake kushindwa vibaya bungeni, Threresa May amesema bado amejizatiti katika kuyatekeleza matokeo ya kura ya maoni ambayo waingereza walipiga mnamo mwaka 2016 kutaka nchi yaom ijiondoe Umoja wa Ulaya..

https://p.dw.com/p/3EvMz
Großbritanien | Theresa May spricht im Unterhaus | Brexit | London
Picha: picture-alliance/dpa/empics/PA Wire/House of Commons

Umoja wa Ulaya umesimama pamoja hata baada ya wabunge wa Uingereza kuukataa tena mpango wa Brexit wa waziri mkuu Theresa May katika kura ya hapo jana. Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamesema Uingereza lazima ijitathmini kwa haki ikiwa kweli inataka kurefusha muda kabla ya kuondoka kwenye Umoja huo.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas amesema hatua ya wabunge wa Uingereza ya kuukataa mkataba juu ya nchi yao kujiondoa kutoka Umoja wa Ulaya ni uzembe. Waziri Maas ameeleza kwamba Umoja wa Ulaya ulipiga hatua ndefu ya kufikia mwafaka na Uingereza juu ya mabadiliko katika mkataba huo. Waziri Maas ametoa kauli hiyo baada ya bunge la Uingereza hapo jana kwa mara nyingine kuukataa mkataba uliofanyiwa mabadiliko na kuwasilishwa kwenye bunge na waziri mkuu Theresa May.

Waziri Maas ameelezea wasiwasi juu ya uwezekano wa Uingereza kujiondoa kutoka Umoja wa Ulaya bila ya mkataba. Ameeleza kwamba yeyote anayeukataa mkataba anayaweka maisha ya raia wake na uchumi wa nchi yake mashakani lakini amesema Ujerumani imejitayarisha kwa hilo.Juu ya kura iliyopigwa Jumatatu kwenye bunge la Uingereza mjumbe mkuu wa Umoja wa Ulaya kwenye mazungumzo ya Brexit Michel Barnier ameitaka Uingereza ijipange vizuri kwa sababu amesema umebakia muda mfupi tu kabla ya kufikia uwezekano wa Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya bila ya mkataba.

Kibonzo cha Theresa May, jinsi alivyoelemewa na mchakato wa Brexit
Kibonzo cha Theresa May, jinsi alivyoelemewa na mchakato wa Brexit Picha: DW/Vladdo

Mjumbe Mkuu wa Umoja wa Ulaya kwenye mazungumzo ya Brexit Barnier ameongeza kusema kwamba, serikali ya Uingereza inapaswa kubadilisha mkakati baada ya bunge kuukataa mkataba uliowailsihwa na  waziri mkuu May. Bwana Barnier amesema, kwa mara yingine bunge la Uingereza limeonyesha kile linachopinga na kwamba mkwamo huo unaweza kuondolewa na waingereza wenyewe tu.

Wabunge 391 walipiga kura kuupinga mkataba uliowasilishwa na waziri mkuu Theresa May. Ni wabunge 242 tu waliouunga mkono. Juu ya matokeo ya kura ya hapo jana kiongozi wa wabunge wa chama cha upinzani cha Labour kwenye bunge la Ulaya Richard Cobert amesema siyo jambo la kushangaza, baada ya kushindwa vibaya waziri mkuu Theresa May alijaribu kuwaliwaza wanasiasa wa mrengo wa kulia ndani ya chama chake lakini ameshindwa na sasa ameanguka kwa kushindwa vibaya sana.

Waziri Mkuu Theresa May atawaomba wabunge wa Uingereza leo Jumatano waamue iwapo nchi hiyo itaondoka Umoja wa Ulaya bila mkataba. Na iwapo wabunge wataamua kama inavyotarajiwa yaani kuunga mkono mswaada wa Uingereza kutoondoka bila ya mkataba waziri mkuu Theresa May ameahidi kura nyingine siku ya Alhamisi juu ya kuurefusha mchakato wa Brexit ambapo itakuwa ni siku 15 tu kabla ya Uingereza kuondoka Umoja wa Ulaya hapo Machi 29. 

Vyanzo: AP/AFP/p.dw.com/p/3Eug5