Uingereza yatakiwa kuweka bayana msimamo wake juu ya Brexit
14 Mei 2018Umoja wa Ulaya umesema Uingereza inapaswa kuhakikisha kuwa haijiondoi kwenye Umoja huo mwezi Machi mwaka ujao bila ya makubaliano, hatua inayoongeza shinikizo kwa Waziri Mkuu Theresa May. Lakini kwa upande wake msemaji wa May, amesema kinachopewa kipaumbele kwa sasa ni kutekeleza jambo hilo kwa makini na sio kukimbizana na muda.
Wanadiplomasia na maafisa mjini Brussels wamesema kumekuwepo na maendeleo kidogo katika majadiliano ya Brexit tangu siku ya mwisho ya mkutano wa viongozi wa Umoja wa Ulaya, na kuanza kutilia mashaka iwapo Umoja huo na Uingereza wataweza kufikia hatua nyengine muhimu katika mkutano wao wa kilele utakaofanyika June 28 na 29.
"Tuna wasiwasi kwamba hakuna msimamo wa wazi kutoka kwa Uingereza, muda unayoyoma, tunahitaji kupiga hatua muhimu lakini hilo halijafanyika, kile kinachotupa sisi wasiwasi hasaa ni suala la Ireland Kaskazini ambapo tunatarajia mchango mkubwa kutoka kwa Uingereza," alisema Waziri wa masuala ya Umoja wa Ulaya wa Ujerumani Michael Roth alipokuwa anawahutubia wenzake mjini Brussels.
Nchini Uingereza kwenyewe Waziri Mkuu Theresa May yupo katika wakati mgumu, huku wafuasi wa Brexit wakitaka kukatizwa kwa mahusiano na Umoja wa Ulaya na watu wengine wanaotaka kuwepo kwa mahusiano ya karibu ya Uingerezana na Umoja huo huku wakihimiza ushirikiano wa karibu wa kibiashara ili kupunguza mgongano wa kibiashara katika siku za usoni.
Hata hivyo msemaji wa May amesema wanafanyia kazi mawazo mawili ya ushirikiano baada ya Brexit.
Chini ya ushrikiano wa kiushuru, Uingereza inaweza kukusanya ushuru kwa bidhaa zinazoingia nchini kwa niaba ya Umoja wa Ulaya na chini ya wazo jengine la mpango makhsusi wa ushuru wa forodha, wafanyabiashara waliyo katika orodha iliyokubalika wataweza kuvuka mipaka kwa msaada wa teknolojia inayojiendesha yenyewe.
Masuala mengine ambayo hayajasawazishwa yanajumuisha dhamana ya wataalamu kutoka nje, makubaliano juu ya ushirikiano wa usalama na biashara baada ya Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya ili kuhakikisha kuwa kuna mpango wa kufuatwa baada ya Brexit mnamoMachi 2019.
Waziri wa Australia Gernot Blumel amesema Ulaya imeweka wazi msimamo wake na anatumai kuwa serikali ya Uingereza wataingia katika majadiliano kamili, akizungumzia malalamiko ya muda mrefu ya Umoja wa Ulaya kwamba Uingereza haijaweka wazi azma yake kwa kina katika majadiliano yake juu ya kujiondoa katika Umoja wa Ulaya.
Mwandishi: Amina Abubakar/AP/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga