Ujerumani: Chama cha SPD kuzungumza kuhusu serikali ya mseto
7 Desemba 2017Chama cha Social Democrats cha hapa Ujerumani bado kiko njiapanda, je kitapaswa kuunda muungano mwingine mkubwa na wahafidhina wa Kansela Angela Merkel? Watu wengi katika chama wana wasiwasi, hata hivyo mkutano wa chama hicho unaofanyika mjini Berin leo utatoa majibu.
Chama cha SPD cha mrengo siasa za wastani za mrengo kushoto bado hakijatulia katika jukumu lake jipya kama chama kikuu cha upinzani nchini Ujerumani. Kilipata uchungu wa kushindwa katika uchaguzi mkuu wa mwezi Septemba na viongozi wa chama walitaka kukiunda chama nje ya serikali.
Lakini kushindwa kwa mazungumzo ya kuunda serikali baina ya chama cha kihafidhina cha Christian Democrats CDU cha Kansela Angela, na chama ndugu cha Bavaria cha Christian Social Unioni CSU, chama rafiki kwa biashara Free Democrats FDP na kile cha kijani, kumewafanya SPD kurejea katika ulingo.
Wajumbe wa SPD kutoa mwelekeo ikiwa wataunda serikali na Merkel
Je wataungana tena na Merkel kama washirika wadogo katika muungano wa vyama vikubwa? Ni swali ambalo wajumbe wa SPD wanapanga kulitolea majibu katika mkutano wa chama hicho unaofanyika leo mjini Berlin. Ikiwa watafanya hivyo, watakuwa na idadi kubwa katika bunge, lakini wengi wanahofia kuwa unaweza kuwa mwanzo wa kuporomoka kwa chama hicho.
SPD tayari imepata kidonge cha uchungu mara mbili. Waliongoza na CDU/CSU kuanzia mwaka 2005 hadi 2009 na hatimaye walipoteza idadi kubwa ya kura wakati wa uchaguzi wa kitaifa uliofuata. Hata hivyo, chama hicho kilijaribu tena bahati yake mwaka 2013 na wapiga kura hawakusamehe.
Katika uchaguzi wa mwezi Septemba SPD ilishinda kwa asilimia 20.5 ya kura, ikiwa ni matokeo mabaya ya uchaguzi katika miaka 154 ya historia ya chama. Ilikuwa ni mshutuko kwa chama ambacho hapo mwanzo kiliwahi kujivunia kua chama cha watu, na kinakutana kwa mara ya kwanza tangu kumalizika kwa uchaguzi.
Martin Schulz alegeza upinzani wa kuunda serikali ya mseto
Wakati huo huo kiongozi wa SPD Martin Schulz ameonekana kulegeza kidogo upinzani wake wa wazo la kuongoza tena kama mshirika mdogo na wahafidhina. Hatua hiyo ilikuja baada ya kuhimizwa na rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeir ambaye aliwahi kukiongoza SPD kabla ya kuondoka katika chama na kuchukua majukumu makubwa ya kuwa mkuu wa nchi.
Schulz hivi karibuni amekiri kuwa anajiandaa kufanya mazungumzo na wawakilishi wa vyama vya CDU/CSU juu ya uwezekano huo. Alidokeza kuwa mazungumzo yatakuwa ni sababu itakayoamua ikiwa SPD itajiunga au la , na mwishowe kuingia katika muungano.
Jambo pekee ambalo ni la uhakika ni kwamba wasiwasi kuhusu muungano hautaweza kuwazuia kuzungumza katika mkutano huo. mbunge wa SPD Marco Bülow alionya kwamba chama kinaweza "kuhatarisha kuwepo kwake" kwa kuingia muungano mkubwa na Merkel. Aliongeza kwamba SPD kina uhakika wa kupoteza wanachama wake wengi ikiwa kitafanya hivyo.
Tawi la vijana la chama hicho maarufu kama "jusos" wanaamini kuwa muungano mpya ni njia mbaya. Watu walipiga kura ya kuuondoa muungano mkubwa madarakani, CDU na CSU si washirika wa kuaminika, na kwamba SPD inahitaji nguvu zake yenyewe ili iweze kujiunda tena "badala ya kupiga mbizi katika utawala unaofuata".
Kabla ya chama kujadili hoja ya kujinga au la na uongozi mpya, kiongozi wake Schulz atatoa hotuba inayosubiriwa kwa hamu. Kwa siku kadhaa zilizopita Schulz amesisitiza mara kwa mara kwamba SPD inafahamu majukumu yake ya kisiasa na kusisitiza kwamba chama chake hakitashinikizwa.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi/DW
Mhariri: Saumu Yusuf