Ujerumani huenda ikaondoa wanajeshi wake Uturuki
16 Mei 2017Takriban wanajeshi 250 wa Kijerumani wapo katika kambi ya jeshi la anga ya Incirlik nchini Uturuki, ukiwa ni mchango wa Ujerumani katika ujumbe wa kijeshi unaoongozwa na Marekani unaopambana na kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS katika nchi jirani ya Syria.
Duru za wizara ya mambo ya nje ya Uturuki zimeliambia shirika la habari la Reuters, kwamba ziara ya wabunge wa Kijerumani katika kambi hiyo haitakuwa hatua sahihi kwa sasa bila ya kutoa maelezo zaidi.
"Hii ni bahati mbaya sana, na tumelisema hilo kwa njia tofauti. Tutaendelea na mazungumzo na Uturuki lakini wakati huo huo tutalazimika kutafuta njia nyingine za kutimiza lengo letu kwa sababu tumeshawahi kuwa na tatizo hili la kuzuiwa ziara, kabla. Na hilo linamaanisha kutafuta njia mbadala kwa kambi hii ya Incirlik na suluhu moja miongoni mwa nyingine ni Jordan," amesema Kansela Angela Merkel, akiwa katika mkutano na waandishi habari hapo jana, alipoulizwa juu ya uamuzi wa serikali ya Uturuki wa kuwazuia wabunge wa Ujerumani kuwatembelea wanajeshi wao katika kambi hiyo ya jeshi la anga ya Incirlik.
Timu ya utafiti wa kijeshi ya Ujerumani itaizuru Jordan katika siku za karibuni kuangalia uwezekano wa kupata kambi ya kijeshi nchini humo. Hayo ni kulingana na duru za serikali ya Ujerumani.
Kutokana na sababu za kihistoria na kama njia ya kuzuia matumizi mabaya ya madaraka, jeshi la Ujerumani Bundeswehr linadhibitiwa na bunge la Ujerumani, na sio serikali, hili linamaanisha kwamba wabunge wana haki ya kukagua shughuli za jeshi la Ujerumani, ikiwa ni pamoja na vikosi vya kijeshi vilivyotumwa nje ya nchi.
Uhusiano kati ya Uturuki na Ujerumani uliporomoka kwa kasi kubwa kuelekea uchaguzi wa kura ya maoni wa Aprili 16 wa nchini Uturuki wa kupanua madaraka ya Rais wa nchi hiyo Tayyip Erdogan.
Ujerumani na washirika wengine wa nchi za Magharini wameonesha wasi wasi kuhusu kile wanachokitaja kuwa ni kuelekea utawala wa kimabavu nchini Uturuki.
Mwaka jana Uturuki iliwaekea marufuku wabunge wa Ujerumani kutembelea kambi hiyo kwa miezi kadhaa ikiwa kama jawabu la azimio la bunge la Ujerumani la kutangaza mauaji ya Waarmenia yaliyofanywa na vikosi vya utawala wa Ottoman mwaka 1915 kuwa ni ya kimbari, matamshi yaliyokataliwa na Uturuki
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani amaesema Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel atalizungumzia suala hilo la kambi ya Incirlik na wenzake ambao pia ni wanachama wa NATO mjini Washington Marekani leo hii.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/rtre/DW
Mhariri:Iddi Ssessanga