Rais wa Uturuki erdogan awasili Ujerumani
17 Novemba 2023Rais Recep Tayyip Erdogan anazuru Ujerumani katikati ya sintofahamu baina ya mataifa hayo mawili, baada ya rais huyo kutoa matamshi makali kabisa ya kuikemea Israel kufuatia mashambulizi yake dhidi ya wanamgambo wa Hamas katika Ukanda wa Gaza, kiasi cha kuiita "taifa la kigaidi".
Erdogan amewasili katika uwanja wa ndege wa kijeshi nje ya mji mkuu Berlin muda mfupi uliopita kwa ajili ya ziara hiyo itakayodumu kwa masaa machache.
Viongozi mjini Berlin wamemkaribisha Rais huyo wa Uturuki kwa mazungumzo, katikati ya sintofahamu iliyochochewa na matamshi yake makali yaliyoitaja Israel kuwa ni "taifa la kigaidi" na kila wakati akiongeza ukosoaji wake dhidi ya Israel, tangu ilipoanzisha mashambulizi ya kisasi dhidi ya Hamas katika Ukanda wa Gaza.
Ikumbukwe Hamas ilifanya shambulizi kubwa la oktoba 7, lililosababisha vifo vya karibu Waisrael 1,200, wengi wao wakiwa ni raia.
Kiongozi huyo wa Uturuki aidha ameishutumu Israel kwa uhalifu wa kivita, uliosababisha vifo vya watu 11,000 wengi wao wakiwa ni raia pamoja na watoto, hii ikiwa ni kulingana na mamlaka zinazotawala Gaza.
Erdogan anazuru Ujerumani baada ya miaka mitatu
Msimamo huo wa Erdogan uliibua maswali mengi nchini Ujerumani kuhusiana na busara ya kumkaribisha wakati huu, huku upande wa upinzani wa kihafidhina na hata wa kiliberali, FDP ambao ni miongoni mwa unaounda serikali ya kansela Scholz , waliohoji kwa nini hakuifuta ziara hiyo?
Soma zaidi: Erdogan ahutubia maandamano ya kuiunga mkono Palestina
Lakini msemaji wa Scholz Steffen Hebestreit amesema kumekuweko na mahusino mabaya baina ya washirika hao wawili ambayo wanalazimika kuyatafutia ufumbuzi, ingawa alikiri kwamba ni ziara ngumu na hasa kwa kuzingatia mazingira yaliyopo.
Hii ni ziara ya kwanza ya Erdogan nchini Ujerumani tangu mwaka 2020, wakati alipohudhuria mkutano kuhusu Libya uliofanyika nchini humo.
Kwenye ziara hiyo Erdogan anatarajiwa kukutana na Rais wa shirikisho la Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier kwenye makazi yake rasmi Schloss Bellevue na kufanya mazungumzo, kabla ya baadae kukutana kwa mazungumzo na kansela wa Ujerumani Olaf Scholz katika hafla ya chakula cha jioni.
Soma zaidi: Erdogan na Netanyahu wakutana kwa mara ya kwanza tangu mahusiano kuingia doa
Suala jingine ambalo huenda Erdogan akaliibua ni matarajio ya Uturuki ya kununua ndege 40 za kivita aina ya Eurofighter Typhoon, ambazo kwa mujibu wa wizara ya ulinzi ya Uturuki, mtengenezaji mwenza ambaye ni Ujerumani anapinga ununuzi huo.
Uhusiano kati ya mataifa hayo mawili mara zote umekuwa mgumu, katika wakati ambapo Berlin ikikosoa vikali hatua kali za Erdogan dhidi ya wapinzani wake wa ndani. Lakini hata hivyo bado Uturuki bado anasalia kuwa mshirika muhimu si tu kwa Ujerumani bali pia Ulaya na Jumuiya ya kujihami ya NATO, na hasa kutokana na ushiriki wake kuanzia kusimamia makubaliano ya usafirishaji wa nafaka kutoka Ukraine katikati ya vita vya Urusi hadi makubaliano muhimu ya kudhibiti mmiminiko wa wahamiaji barani Ulaya kati ya mwaka 2015-16.
Erdogan anatarajiwa kurejea Uturuki kesho usiku wa leo.