Ujerumani yaendelea kuinyima silaha Saudi Arabia
24 Machi 2020Mgogoro huo unaoelezewa kuwa ni vita vya kiwakala kati ya majeshi ya serikali ya Yemen yanayoungwa mkono na Saudi Arabia yanayopambana na waasi wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran umesababisha hali mbaya nchini humo. Kutokana na hali hiyo asilimia 80 ya wananchi wapatao milioni 24 sasa wanategemea misaada ya kimataifa.
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia mgogoro wa Yemen Martin Griffiths amesema uwezekano wa nchi kadhaa kuhusika moja kwa moja kwenye mgogoro huo umezidi kuwa mkubwa.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limetilia maanani mashambulio ya anga yanayofanywa na vikosi vinavyoongozwa na Saudi Arabia yanayosababisha vifo vya maalfu ya watu na sehemu nyingi za kiraia. Asasi hiyo ya hali za binadamu imesema mashambulio hayo yanakiuka sheria za kimataifa kuhusu vita.
Maafa makubwa kwa watoto
Wakati huo huo shirika la kutetea haki za watoto Save the Children limesema vita vya nchini Yemen vimesababisha maafa makubwa kwa watoto hasa afya yao ya kiakili. Majeshi ya serikali ya Yemen yanayoungwa mkono na mfungamano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia yamekuwa yanapambana na waasi wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran kwa muda wa zaidi ya miaka mitano na mpaka sasa hakuna dalili ya mgogoro huo kumalizika.
Na katika juhudi za kimataifa za kujaribu kuutatua mgogoro huo serikali ya Ujerumani imesimamisha kupeleka silaha kwenye nchi zinazohusika katika mgogoro wa Yemen. Uamuzi huo umeafikiwa na vyama vinavyoongoza serikali na hatua hiyo itaihusu Saudi Arabia mnunuzi mkuu wa silaha kutoka Ujerumani.
Uamuzi huo utaanza kutekelezwa mara moja. Umoja wa mataifa umezilaumu pande zote zinazohusika katika mgogoro huo kwa kukikuka haki za binadamu na kwamba pande hizo zinaweza kukabiliwa na mashtaka ya uhalifu wa kivita.
Vyanzo; AFP, DW