Ujerumani kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na India
6 Juni 2023Ujerumani inataka kuongeza ushirikiano wa kijeshi na India. Akizungumza wakati wa ziara yake mjini New Delhi, Waziri wa Ulinzi Boris Pistorius amesema kuwa ni wakati wa kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kati ya nchi hizo mbili. Alikutana na wawakilishi wa sekta ya silaha ya Ujerumani, ambayo inataka kupanua ushirikiano wake na India. Pistorius alisema suala lililopo mezani kwa sasa ni mpango wa dola bilioni moja wa kuiuzia India nyambizi za Kijerumani. Amesisitiza kuwa India ni mshirika muhimu wa Ujerumani katika kanda hiyo licha ya kuwa haijachukua msimamo wa wazi kupinga vita vya Urusi nchini Ukraine. India ambayo ina idadi ya watu bilioni 1.4, ina moja ya majeshi makubwa zaidi duniani na ni mojawapo ya waagizaji wakubwa zaidi wa vifaa vya kijeshi.